Kwa miaka mingi wananchi wa kijiji cha Lunyere-Dar Pori katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamekuwa wakipata shida ya kusafiri umbali mrefu wa kufuata matibabu katika kituo cha afya cha Mpepo kilichopo wilayani mbinga kutokana na zahanati ya kijiji hicho kukosa vitendea kazi mbalimbali vya kuhudumia wagonjwa ikiwemo Darubini, vitanda na magodoro ya kulaza wagonjwa.
katika hali ya kushangaza zahanati hii ya Lunyere-Dar Pori wilayani Nyasa, mbali ya kushindwa kulaza wagonjwa kwa kukosa vitanda na magodoro pia haina Darubuni, baadhi ya vifaa tiba navyo vinahifadhiwa sehemu isiyo salama lakini pia chumba cha kujifungulia akina mama sakafu yake imegubikwa na vumbi.
Kwa kutambua mateso wanayopata wananchi kupata huduma za afya, Bwana Cassian Njowoka ambaye pia ni kamanda wa vijana-CCM wilaya ya Nyasa, akaungana na familia yake kukabidhi vitanda 20, magodoro 20, vyandarua 20 pia akaahidi kukarabati chumba cha kujifungulia akina mama wajazito kwa kutoa maru maru Box 20 ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa kwa marehemu Kepten John Komba aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kabla hajafariki.
Mama huyu Omega Mkapunda ambaye kwa mara ya kwanza ameanza kutumia vitanda hivyo kwa kulazwa na mtoto wake anaungana na wananchi wa Lunyere-Dar Pori kuishukuru familia ya bwana njowoka kutekeleza ahadi waliyoitoa kwa mbunge marehem Kepten John Komba.
Pamoja na wananchi hao kuandaa misa maalum katika kanisa katoliki la Dar Pori ya kumkumbuka marehemu Kepten John Komba aliyefariki februali 28 mwaka huu,Bwana Njowoka pia ameahidi kuihudumia zahanati hiyo kwa kutoa madawa yenye thamani ya shilingi milioni moja kila mwaka pamoja na kutoa nusu ya gharama ya kununulia Darubini.