Tuesday, April 14, 2015

VVU TOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO



VVU TOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO
Kwa kawaida, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU) yanaweza kutokea kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.



Tangu Ugonjwa Unaodhoofisha Kinga ya Mwili (Ukimwi) ulipogundulika mwaka 1983, zimekuwapo changamoto kuhusu maambukizi hayo. Kubwa ni maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

Kwa kawaida, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU) yanaweza kutokea kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hali hii inaweza kutokea kwa njia kuu tatu; wakati wa ujauzito, uchungu na kujifungua na baada ya kujifungua kwa njia ya kunyonyesha.

Kama hali hii isipodhibitiwa, uwezekano wa kutokea maambukizi ni kati ya asilimia 20 mpaka 45. Kwa vigezo vyovyote vile idadi hii ni kubwa na kazi ya Mpango wa Kitaifa Kudhibiti hali hiyo (PMTCT) ni muhimu.

Asilimia tano mpaka kumi ya maambukizi hutokea wakati wa ujauzito wenyewe, asilimia kumi mpaka kumi na tano wakati wa uchungu na kujifungua na asilimia tano mpaka ishirini wakati wa kunyonyesha.
 
Vipo vipengele mchanganyiko na hatarishi ambavyo kuwepo kwake kunaongeza uwezekano wa VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wake.

Wingi wa virusi kwenye mwili wa mama, kiwango kidogo cha chembechembe za CD4 hali ambayo hutokea kwa wale wanaopata maambukizi kwa mara ya kwanza na wale walio kwenye hatua za mwisho za maambukizi (AIDS) ni sababu mojawapo.

Kiwango cha maambukizi na ukali wake pia hutegemea na aina ya virusi. Uwezekano wa maambukizi na kiwango chake viko juu zaidi kama mama ana virusi vya HIV-1 kuliko aliye na aina ya HIV-2 .

Kwa bahati mbaya kirusi cha HVI-1 ndicho kinachopatikana zaidi Afrika.
Maambukizi ya bacteria, malaria na magonjwa ya zinaa husababisha kondo la nyuma kupitisha VVU kwa urahisi zaidi wakati wa ujauzito.

Kupasuka kwa chupa zaidi ya saa nne wakati wa uchungu na kujifungua pia huchangia maambukizi kutokea kwa kiwango kikubwa na hasa kama kuna maambukizi kwenye mfuko wa uzazi.

Vipengele vingine hatarishi hutokana na wakati wa kunyonyesha kama magonjwa ya kinywa kwa mtoto, matiti kuwa na vidonda au majipu, muda wa kunyonyesha na kutumia chakula mchanganyiko na na maji kabla mtoto hajatimiza umri wa miezi sita.