Mamlaka ya mapato tanzania TRA imekamata makontena nane yaliyokuwa yamekwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia tatu baada ya kutoa nyaraka zinazoonyesha bidhaa zilizomo ndani yake ni unga wa jipsam ambao kodi yake awali mmiliki wa makontena hayo alikuwa alipie shilingi milioni 20 tu.
Waziri wa fedha Mh.Saada Mkuya amekagua makontena hayo yaliyohifadhiwa eneo la bandari kavu kurasini na kubaini baadhi ya bidhaa zilizokuwa ndani ya makontena hayo ambazo ni vitenge,vipuri vya pikipiki,maziwa na TV na kuongeza kuwa mtuhumiwa atalipa kodi inayostahili pamoja na penati na baadae hatua za kisheria zitachukuliwa.
Kwa upande wake kamishna wa forodha Bw.Tiagi Kabisi amesema makontena hayo yamegundulika baada ya kupita kwenye mfumo maalumu wa TRA ambao una uwezo wa kugundua bidhaa zilizopo kwenye makontena na kwamba bidhaa zote hizo viwango vyake vya kodi ni vikubwa tofauti na vya unga wa jipsam huku akidai kuwa sheria za nchi haziruhusu kutaja jina la mmliki au kampuni yenye mali hadi atakapofikishwa mahakamani.
Akizungumzia mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea nchini waziri mkuya amesema serikali inaangalia hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaoendelea na mgomo huo kwani wamekuwa wakisababisha usumbufu mkubwa siyo tu kwa wananchi bali hata kwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ambapo ITV imetembelea maeneo ya kariakoo jijini Dar es salaam na kushuhudia maduka yakiwa yamefungwa.