Tuesday, April 07, 2015

NYUFA ZA TAIFA ZINAZIDI KUONGEZEKA; NI HATARI!




NYUFA ZA TAIFA ZINAZIDI KUONGEZEKA; NI HATARI!
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
Eric Shigongo
Mungu ni mwema sana hivyo wote tuseme; ahimidiwe daima.
Mara kwa mara nimekuwa nikiwaambia wananchi kupitia safu hii kwamba kinachoonekana sasa katika nchi zenye machafuko hazikuanza siku moja. Zilianza hatua kwa hatua na baadaye nje ya nchi hizo walimwengu wakasema nchi fulani ina machafuko.
Nchi yetu tayari tumetimiza miaka zaidi ya 50 tangu kupata uhuru. Na tujiulize; je bado tumesimama kama taifa imara lenye umoja, mshikamano na amani? Msingi mkuu wa umoja wetu, kama ulivyojengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ulikuwa ni usawa na haki kwa wote. Je, leo tunaweza kuendelea kujivunia hayo au na kama hatuwezi kujivunia nani alaumiwe? Hapana lina nyufa nyingi za hatari, ufisadi, udini, rushwa, uonevu na kunyima haki watu na kadhalika.
Leo nijadili ufa wa ufisadi. Nakumbuka  Aprili 14, 2000, Jaji Joseph Sinde Warioba wakati akifungua warsha ya maadhimisho ya miaka 79 ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere alitaja nyufa kubwa zilizokuwa zimejitokeza na kutishia umoja wa kitaifa. Miaka kadhaa baadaye si tu kwamba nyufa hizo zimezidi kupanuka na ipo ya udini sasa Tanzania imo hatarini.
Jaji Warioba wakati ule alizungumzia ufa wa kukithiri kwa ufisadi nchini akasema hivi: "Kuna mwenendo usiopendeza wa kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya  matajiri na maskini. Siasa imetekwa na matajiri kwa kushirikiana na wasomi. Ufisadi na rushwa sasa ni vitu muhimu katika uchaguzi na si sera…..ufisadi unaigawa vipande jamii. Tunauzungumzia sana, tunaushutumu sana, lakini pia tunashiriki bila haya kuuendeleza."
Tujiulize zaidi ya miaka nane sasa tangu  Jaji Warioba atoe kauli hiyo, hali ikoje? Kwa kuzingatia kashfa chache zilizoibuliwa za miaka ya hivi karibuni za IPTL, ununuzi wa rada, EPA, Richmond, Kiwira, Songas, Buzwagi, majengo ya BOT na hata uuzaji wa nyumba za serikali, Escrow ni wazi hali ni mbaya zaidi, na kama ni ufa katika nyumba, basi, mtu akiwa nje anaona kilichopo ndani!
Hali hiyo ya wasomi kufungamana na wafanyabiashara na 'kuiteka' siasa ndiyo chimbuko la kuongezeka kwa ufisadi nchini.Tumefika mahali ambako hivi sasa wengi wanaojitosa kugombea uongozi ni wale wenye pesa nyingi za kuhonga  na wakishashinda hupanga namna ya kurejesha.
Nikilitafakari jambo hili, ndivyo ninavyozidi kuamini kwamba ni wafanyabiashara ndiyo  waliofanikiwa kumshawishi Rais Benjamin Mkapa kujitosa katika biashara angali ikulu. Siamini kwamba mzee Mkapa wa mwaka 1995 alikuwa akitamani kuwa milionea na kuamua kufuata njia ya mkato kwa kununua Machimbo ya Makaa ya Mawe ya Kiwira!
Ninaweza kuapa kwamba haraka ya kuwa tajiri ambayo Mkapa aliionyesha miaka yake ya mwisho ikulu, ina uhusiano na kuwa kwake karibu na baadhi ya wafanyabiashara akiwasahau wakulima na wafanyakazi.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alituonya zamani kabisa kuhusu suala la chama kuwasahau wakulima na wafanyakazi na badala yake kuwakumbatia matajiri katika hotuba yake aliyoitoa Oktoba 22, 1987 kwenye mkutano wa taifa wa CCM.
Alisema hivi: "Utajiri unaotokana na wizi wa mali ya umma na wizi wa fedha za kigeni na unyonyaji na uharamia wa aina mbalimbali, hautupunguzii umaskini wetu, bali unauongeza. Chama chetu hakiwezi kuwakubali matajiri wa aina hiyo na kikaendelea kuwa CCM, na wala wasitarajie kuwa wananchi watakikubali."
Lakini si Nyerere tu aliyeonyesha hofu ya matajiri hao kukivamia CCM; kwani hata Mkapa na Kikwete walizungumzia pia hofu hiyo katika hotuba zao ndefu za kwanza baada ya kushinda urais (1995 na 2005).
Tatizo ni kwamba ingawa wote wamezungumzia kukerwa na wingi wa matajiri hao wanavyohonga kuwania uongozi, hakuna aliyekwenda mbali zaidi na kuidhibiti hali hiyo ndiyo maana zikatokea kashfa za EPA, Kiwira, Buzwagi, Richmond, Escrow inayowakera wananchi.
Kwa hakika, haiingii akilini kwa serikali kumchangisha maskini pesa za ujenzi wa maabara wakati inaachia vigogo wanachoteana mabilioni ya shilingi yaliyohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pesa ambazo zingetosha kujenga maabara bila kumchangisha maskini yeyote.
Hali ilivyo sasa kati ya wachota fedha za umma na maskini ni sawa na mke wa Mfalme Louis wa 16 wa Ufaransa, Marie Antoniette ambaye aliishi maisha ya kifahari na kushindwa kuona dhiki za Wafaransa wengine kiasi kwamba aliposikia watu wanalalamika kwa kukosa mikate akasema wapewe keki! Ukweli ni kwamba Bunge letu limechelewa kuisimamia serikali kuhusu ufisadi.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.