Tuesday, April 21, 2015

Mtanzania asimulia vurugu Afrika Kusini....Asema Walengwa wakuu walikuwa Wanigeria, Wasomalia, Wachina



Mtanzania asimulia vurugu Afrika Kusini....Asema Walengwa wakuu walikuwa Wanigeria, Wasomalia, Wachina
Wakati serikali ikitangaza kuwarejesha Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye moja ya makambi yanayowahifadhi raia wa kigeni walioathirika na vurugu zilizohusisha mauaji, uporaji na watu kukimbia makazi nchini Afrika Kusini, Mtanzania aliyeko nchini humo, amesimulia jinsi raia wengi wa kigeni walivyoathirika.

Joseph Moses, anayeishi mjini Durban, amesema pamoja na baadhi ya raia wa kigeni kuawa, lakini waliothirika hadi sasa wengi wao hawajui watalipwaje mali zao zilizopotea katika ghasia hizo.

Moses, amesema kuna Watanzania wengi mjini Durban wamepoteza mali zao katika vurugu hizo na hawajui watalipwaje.

Hata hivyo, alisema raia wa kigeni walioathirika zaidi na ghasia hizo ni wanaotoka katika nchi za China, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nigeria na Somalia, baada ya maduka pamoja na nyumba wanazoishi kuvamiwa na watu wanaosaidikiwa kuwa ni raia wa Afrika Kusini na kuporwa.

"Kinacholeta utata ni kwamba, hata kama fidia itatolewa haijulikani itakuwaje," alisema Moses na kuongeza kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi katika mji wa Durban ambao umeathiriwa zaidi na vurugu hizo.

Alisema jana ulifanyika mkutano uliomhusisha Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Chifu wa Wazulu, Goodwill Zweluthini anayetuhumiwa kuchochea vurugu hizo na viongozi wengine nchini humo katika kambi ya waathirika hao  mjini Durban.

Moses alisema katika mkutano huo, Chifu Zweluthini aliwapiga marufuku raia wa Afrika Kusini kuendelea kuwashambulia raia wa kigeni.

Alisema sababu iliyotolewa na Chifu Zweluthini ni kwamba, nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, ziliwasaidia weusi wa nchi hiyo kuondoa siasa ya ubaguzi wa rangi.

Hata hivyo, alisema hakuna Mtanzania aliyeuawa katika vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya raia wanane wa kigeni.

Kauli ya  CUF 
Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinasikitishwa na machafuko yanayoendelea nchini Afrika Kusini dhidi ya wakazi wasio wenyeji wa nchi hiyo, wakiwamo Watanzania.

"Haingii akilini hata kidogo baada ya muda mrefu kupambana na makaburu kusaka uhuru wa Afrika leo hii waafrika tunaanza kufukuzana wenyewe," alisema Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdallah Mtolea.

Aliongeza: "Ni wakati, ambao Waafrika Kusini wanapaswa kujua kuwa si wao wanaopoteza ajira tu kwa kuwapo wageni nchini kwao, bali hata mataifa mengine kama Tanzania pia ajira za raia wake zinapotea kwa kuwapo wageni kutoka Afrika Kusini lakini tunavumiliana na hivyo ndivyo tunapaswa kuishi."

Aliitaka serikali ya Afrika Kusini kuongeza nguvu na kuharakisha kukomesha vitendo vya kibaguzi, hasa kwa wageni wanaotoka nje ya nchi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa vyombo vya habari, Chifu Zweluthini amekuwa miongoni mwa wachochezi wa kushambuliwa na kufukuzwa wageni nchini humo.

"Ni wajibu wa serikali ya Afrika Kusini kumwajibisha kisheria ili matendo haya yasiendelee.

Tukizuia isitokee Afrika Kusini tutakuwa tumesaidia hali kama hii isitokee nchi nyingine za Afrika," 
alisema Mtolea.

Alisema CUF ina taarifa kuwa Watanzania walioko Afrika Kusini ni miongoni mwa waliojeruhiwa na kufanyiwa vurugu.

"Kuna fununu ya Watanzania wawili kufariki dunia. Tunaitaka serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Afrika Kusini kuthibitisha hili ili kuondoa wasiwasi," alisema Mtolea.

Aliongeza: "CUF tunajua ni wajibu wa kila Mtanzania kumlinda Mtanzania mwenzake. Na ni wajibu wa serikali kulinda raia wake popote pale walipo duniani. Serikali ya Tanzania haionyeshi kama inawashughulikia Watanznaia walioko Afrika Kusini. Tunaitaka serikali kubeba jukumu la kuwarudisha nyumbani mara moja Watanzania walioko hatarini nchini Afrika Kusini."