NA BASHIR YAKUB-
Kifungu cha 18 cha Sheria ya Kanuni za adhabu sura ya 16 kimeeleza hatua ya mtu kujikinga mwenyewe, kumkinga mwenzake , mali yake mwenyewe na mali ya mwenzake.
Kujikinga( defence) maana yake ni kujilinda au kujitetea inapokwa imekutokea dharula ya kuvamiwa na mtu au watu waovu.
Uovu ni uovu si lazima awe mwizi . Hata mtu asiyekuwa mwizi lakini amekuvamia kwa nia ovu iwe nyumbani, kazini au sehemu nyingine yoyote basi ni adui unayepaswa kujikinga naye.
1.KUJIKINGA NI HAKI YA KILA MTU.
Haki ya kujikinga na adui si tu imeelezwa katika kifungu nilichotaja bali pia ni haki ya msingi ya kikatiba.
Haki hii pia huingia katika zile haki ambazo huitwa haki za kuzaliwa ( in born right). Haki za kuzaliwa ni zile haki ambazo sio lazima ziwe zimeandikwa katika sheria fulani halafu ndipo mtu azitekeleze .
Ni haki ambazo hata kama hazikuandikwa popote mtu ni lazima azipate tu. Kwa mfano haki ya kula au ya kuishi.
Haihitaji iwe imeandikwa popote katika katiba au penginepo ili uweze kula au kuishi.
Ni kitu ambacho hutokea moja kwa moja( automatic). Ni kitu ambacho huandikwa kama haki katika sheria lakini hata kisingeandikwa ilikuwa ni lazima kiwepo.
Halikadhalika ndivyo ilivyo katika haki ya kujikinga ( defence) kwani haihitaji kuwa imeandikwa popote kuwa mtu akikuvamia kukudhuru ujikinge naye.
Inakuja tu moja kwa moja mtu akitaka kukudhuru ni lazima ujilinde kwa kutafuta namna ya kujiepusha naye.
2. INARUHUSIWA KUJIKINGA HADI KUUA.
Kifungu cha 18c cha sheria hiyohiyo ya kanuni za adhabu kinasema kuwa mtu anaweza kujikinga mwenyewe, mali yake , kumkinga mtu mwingine, mali ya mtu mwingine dhidi ya hatari au shambulio mpaka kufikia hatua ya kuua au kusababaisha madhara makubwa ya kimwili.
Madhara makubwa ya kimwili ni pamoja na kukata kiungo cha mtu mfano mguu, mkono, au kusababnisha madhara mengine kama kusababisha kidonda kikubwa na hali nyingine zote zinazofanana na hizo.
3. ANAYEUA AU KUSABABISHA MADHARA MAKUBWA KWA MTU MWINGINE KATIKA KUJIKINGA HANA KOSA KISHERIA.
Mtu yeyote anapokuwa katika harakati za kujikinga au kumkinga mtu mwingine na adui halafu akaua au akasababisha kifo kisheria anakuwa hana kosa na hapaswi kushitakiwa na hata akishitakiwa basi utetezi wake ( defence) itakuwa ni kusema kuwa alikuwa katika harakati za kujikinga, kumkinga mtu au mali.
4. BAADHI YA MAKOSA AMBAYO UKITENDEWA WAWEZA KUUA KATIKA KUJIKINGA.
Kifungu hicho cha 18C ( a – e) kimetaja baadhi ya makosa ambayo ukitaka kutendewa, au mtu mwingine kutendewa basi yafaa kujilinga hadi kuua au kusababisha kifo.
Baadhi ya makosa hayo ni kubaka, kulawiti, Kunajisi, jaribio la kuua, shambulio lolote linalolenga kusababisha madhara makubwa ya kimwili, utekaji nyara, wizi wa silaha, kuchoma moto, na makosa mengine yote ambayo yanalenga kusababisha uharibifu mkubwa katika mali.
5. MAANA HALISI YA KUJIKINGA HADI KUUA.
Kujikinga hadi kuua mfano wake ni huu, mtu amekuvamia nyumbani mchana au usiku na lengo lake ni kukuua kwakuwa tayari ameshikilia upanga.
Katika mazingira kama hayo basi na wewe waweza kuchukua upanga au namna nyingine yoyote kumuwahi kabla hajakukata wewe.
Au mkabaji amekukaba usiku au mchana lengo ikiwa akuibie na amekukaba kiasi usipofanya jitihada anaweza kukusababishia kifo.
Katika mazingira kama hayo kama utapata nafasi ni ruhusa kupiga popote au kutumia chochote kumuua ili upate kupona wewe. Katika mazingira yote hayo niliyoeleza huna shitaka la kujibu mbele ya sheria.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com