Monday, April 20, 2015

KIKWETE KUWATUNUKU WALIONG´ARA 7 KIDATO CHA NNE 2014


KIKWETE KUWATUNUKU WALIONG´ARA 7 KIDATO CHA NNE 2014
RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kutoa zawadi kwa wanafunzi, shule, halmashauri na mikoa iliyofanya vizuri katika ufaulu katika mitihani ya Darasa la Saba na Kidato cha Nne mwaka 2014.


Akizungumza jana Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema zawadi hizo zitatolewa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu Mei 15 mwaka huu mjini Dodoma.
"Wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Rais Jakaya Kikwete anatumia fursa hiyo kuzungumza na wananchi na pia kutoa zawadi kwa waliofanya vizuri katika mitihani ya mwaka 2014," alisema.
Mchome alisema uzinduzi wa maadhimisho hayo kitaifa utafanyika Mei 11 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma yanayokwenda sambamba na maonesho ya shughuli mbalimbali za wadau wa elimu yatafunguliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Maadhimisho hayo yanayofanyika kwa mara ya pili ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa– Big Results Now ( BRN ) katika Sekta ya Elimu.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne 2014, yalionesha ufaulu wa watahiniwa wote wa shule na kujitegemea ukipanda kwa asilimia 10.8 huku watahiniwa 73,832 walipata madaraja ya Distinction, Merit na Credit.
Kwa upande wa matokeo ya darasa la Saba 2014, ufaulu wa kimasomo, umepanda kwa asilimia kati ya 0.64 na 8.94 ikilinganishwa na mwaka 2013.