Tuesday, April 14, 2015

JIJI LA NAIROBI LAKANUSHA KUZIKA MAITI ZA GARISSA KABURI MOJA



JIJI LA NAIROBI LAKANUSHA KUZIKA MAITI ZA GARISSA KABURI MOJA
Wafanyakazi wa shirika la kujitolea la Msalaba Mwekundu nchini Kenya wakipanga majeneza yenye miili ya marehemu wa shambulio la Garissa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Chiromo jana.
HALMASHAURI ya jiji la Nairobi imekataa ripoti kwamba jana iliwazika wanafunzi waliouawa katika mashambulizi ya kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garissa kiasi cha wiki mbili zilizopita, kwenye kaburi la pamoja.
Akizungumza katika ofisi za jiji hilo, Ofisa Uhusiano, Beryl Okudi, alisema serikali haina habari  kuwa miili ya watu hao ilikuwa inatolewa kwenye chumba cha maiti cha jiji hilo.
 "Hilo ni jukumu la serikali kuu.  Hakuna miili ya waliouawa Garissa iliyopelekwa kwenye chumba cha maiti cha halmashauri ja jiji hili.  Miili yote ilipelekwa chumba cha maiti huko Chiromo," alisema Okundi.
Jana kulikuwa na habari kwamba magari ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) yalikuwa yanasomba maiti kuzipeleka kwenye Makaburi ya Lang'ata.
Hii ni baada ya picha mbalimbali kuhusu jambo hilo kuwekwa kwenye mitandao na watu kushangaa kwa nini miili hiyo ilikuwa inadhalilishwa.
CHANZO: THE STAR