Viongozi waliozuiliwa ni Mbunge wa Muleba kusini Profesa Anne Tibajuka,Mbunge wa Bariada Magharibi Adrew Chenge pamoja Mbunge wa Sengerema William Ngeleja ambao wote kwa pamoja waliingiziwa pesa na Mbia wa kampuni ya IPTL bwana james Rugimalira kupitia Akaunt ya Benki ya Mkombozi.
Akitangaza Maazimio hayo ya Kamati ya CC yaliyotokana na kikao kilichofanyika kwa siku moja Mkoani Dar Es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM,Nape Nnauye wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari amesema Kamati kuu ya CCM (cc) imelijadili suala hilo kwa makini na kuwazuia viongozi hao wasiingie kwenye vikao hivyo
"Tumewataka viongozi hawa waliohusika na mihamala ya Akaunt ya Escrow ambao ni viongozi,akiwemo mama Tibaijuka ambaye naye ni mjumbe wa CC,Andrew Chenge mjumbe wa Nec na Ngereja pia ni wa Nec wasiingia kwenye vikao hivyo mpaka pale suala hilo litakapotafutiwa ufumbuzi"amesema Nape.
Nape Ameongeza kuwa suala lao litajadiliwa na Kamati ndogo ya Maadili ya Chama hicho ambayo itachunguza na kupeleka majibu haraka kwenye kamati kuu CC na kutolewa majibu.
Aidha,Kamati kuu hiyo ya CCM yaani CC imewarushia mzigo Kamati ya Maadili ya chama hicho kuangalia adhabu ya Makada wake waliotangaza nia mapema kama walikiuka adhabu waliyopewa ya kufungiwa kwa miezi 12 kwa makada Sita wa chama hicho walioanza kampeni mapema ya Urais ndani ya chama hicho kabla ya mda kuanza.
"Kuhusu makada wetu waliotangaza nia mapema ya kutangaza uongozi mbalimbali hususani Urais, tumeiachia Kamati ya Maadili kuangalia kama walikiuka adhabu waliyopewa au hawakukiuka. Kamati hiyo inatakiwa itutoe majibu" amesema Nape.
Alibainisha kuwa Kamati hiyo ya Maadili imeambiwa ianze kazi mara moja na ipeleke majibu kwenye kamati Kuu.
Makada hao waliokuwa chini ya adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
Vilevile baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kutokana na adhabu ya onyo kali makada hao kwa mwaka mzima walikuwa katika hali ya kuchunguzwa ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Vilevile Chama hicho kimepokea kwa masikitiko Makubwa Msiba wa Mbunge wa Mbinga Mashariki Kaptain John Komba na kusema ni pengo kubwa sana.