Thursday, March 12, 2015

Majeruhi wa Basi Lililoua Watu 42 LEO Wazungumzia UKAIDI Wa Dreva wa Basi Hilo



Majeruhi wa Basi Lililoua Watu 42 LEO Wazungumzia UKAIDI Wa Dreva wa Basi Hilo


Watu arobaini na wawili wamefariki dunia huku ishirini na wawili wakiwa wamelazwa hospitalini baada ya ajali ya barabarani iliyotokea asubuhi ya Jumatano, Machi 11, 2015 huko katika eneo la Changarawe, Mufindi katika mkoa wa Iringa.
 Taarifa zaidi kutoka kwa watu walio katika eneo hilo zinasema kuwa miili ya maiti 32 bado haijatambuliwa na ndugu ama jamaa.


Mkuu wa polisi katika mkoa wa Iringa, ameelezea chanzo cha ajali hiyo akibaini kwamba dereva wa lori alijaribu kukwepa moja ya shimo katika barabara suala lililomsababisha kutoka katika upande wake wa barabara hadi upande wa basi hilo na kusababisha kugongana na basi hilo la kampuni ya Majinja Express.
  
Moja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Jackson Manga amesema kama dereva wa basi hilo angezingatia ishara za taa kali alizokuwa akiwashiwa na dereva wa lori hilo kwa vyovyote vile ajali hiyo isingetokea. Manga amesema katika eneo hilo lenye mteremko wa wastani, lori lilikuwa likipandisha na basi lilikuwa likishuka.


Amesema ukaidi wa dereva wa basi ulisababisha dereva wa lori aingie katika shimo kubwa katika eneo hilo hali iliyosababisha ashindwe kulimudu gari hilo kabla ya kuvaana uso kwa uso na basi hilo.

"Baada ya kuvaana, kontena la futi 40 lililokuwa limepakiwa katika loli hilo liliruka juu na kwa kishindo kikubwa, kubamiza na kufunika basi," alisema.


Mmoja wa majeruhi wa basi hilo, Kevin Humphrey ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi amesema; "Tulisikia mshindo mkubwa baada ya basi letu kugongana na lori hilo na mshindo huo ulisababisha na kontena iliyotoka kwenye lori hilo na kupiga juu ya basi letu."