Polisi kwa kutumia kikosi cha FFU jana kilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi na wamachinga wenye hasira waliokwenda kubomoa uzio uliojengwa usiku na wafanyabiashara wenye asilia ya ki-Asia kuzuia wananchi wasikatishe mtaa wa Makoroboi, jijini hapa.
Akizungumza jana, Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha, alisema ofisi yake haina taarifa yoyote kuhusu kujengwa kwa uzio uliobomolewa na wananchi hao.
"Hapa nilipo nasubiri nipate taarifa kutoka kwa mhandisi ama mkurugenzi wa jiji kama kulikuwa na kibali kinachoruhusu ujenzi wa uzio kujengwa kati ya makutano ya mtaa wa Makoroboi na Nyerere pamoja na Mzambarauni," alisema Kotecha.
Hata hivyo, alisema hawezi kuzungumzia zaidi vurugu hizo kutokana na kutofahamu lolote licha ya kutokea katika kata yake ya Nyamagana.
Kutokana na hatua ya polisi jijini Mwanza kutumia mabomu ya machozi kila wakati, wakazi wa jiji hilo wamesema wamechoshwa na hali hiyo kutokana na kushindwa kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato.
Naye Sebhi Majura akizungumza kwa niaba ya wananchi, alisema wananchi wa jiji la Mwanza wamechoshwa na matumizi ya mabomu ya FFU kila mara kutokana na kushindwa kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato.
"Hivi uchumi wa mkoa ama taifa utaongezekaje iwapo mambo kama haya ya kutumia mabomu ya machozi yataendelea kufanyika kila siku, nani atazalisha uchumi," alihoji Majura.
Aidha, alisema uzio uliojengwa usiku wa manane na wafanyabiashara wa ki-Asia wanaozunguka eneo hilo, inaonyesha wametumia nguvu ya pesa ili kuwakandamiza wananchi wa kawaida wasifanye shughuli zao mtaa wa Makoroboi.
Majura alisema uzio uliojengwa kwa ajili ya kuzuia kuingia ama kutoka mtaa wa Makoroboi, ni jambo la kushangaza kutokana na barabara hiyo kuwapo kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika.
Hata hivyo, Marwa Magandiko, alisema walinzi wanaolinda maduka ya Makoroboi, walimpigia simu saa 6 usiku na kumfahamisha jinsi ujenzi wa haraka haraka wa uzio unavyoendelea kuziba mtaa huo.
"Tulifika eneo hilo saa 12 asubuhi na kushuhudia jinsi ambavyo uzio umejengwa na kuwekwa geti ili watu wengine wasipite…wananchi wenye hasira walivunja hadi alipofika mkuu wa kamanda wa polisi wilaya ya Nyamagana," alisema Magandiko.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nyamagana, Ally Kitumbo, akizungumza na wananchi, alisema ni kosa la kisheria mtu kuharibu mali ya mwingine bila kufuata utaratibu.
"Wananchi hawa walitakiwa kufuata utaratibu iwapo uzio huu umejengwa ukiwa na kibali ama la, lakini kuharibu mali ya mwingine ni kosa la kisheria," alisema.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema atalizungumzia tukio hilo baada ya kuwasiliana na uongozi wa Jiji la Mwanza ili kufahamu ujenzi huo ulikuwa na kibali ama la.