Saturday, March 14, 2015

MAAFA MWANZA-NILIOKOA WAJUKUU 50 NIKAPOTEZA WATANO ASEMA BABA MWENYE FAMILIA YA WATU 70.


MAAFA MWANZA-NILIOKOA WAJUKUU 50 NIKAPOTEZA WATANO ASEMA BABA MWENYE FAMILIA YA WATU 70.

Kahama. "Kwanza nilikuwa nakwenda Didia Ruhumbo, Wilaya ya Shinyanga Vijijini nikajaza mafuta kwenye gari yangu, lakini nafsi yangu iligoma nikarudi nyumbani nikapaki gari nikawa nimetulia…," anasema mkazi wa Kijiji cha Mwakata, Donald Lubunda (64), baba mwenye familia ya watu 70.


Familia ya Lubunda ni miongoni mwa zilizoathiriwa na maafa ya mvua, ambayo imeacha msiba mkubwa kwenye familia yake baada ya kupoteza na watu watano huku akishuhudia.
Katika tukio hilo, Lubunda alipoteza mtoto mmoja na wajukuu wanne, wawili waliangukiwa na ukuta na wengine kupigwa mawe ya mvua hadi kufa, huku jitihada zake zikifanikisha kuokoa wengine 50.
"Nilikuwa naingia kulala baada ya kuahirisha safari yangu, ghafla wingu zito lilitanda kuonyesha dalili ya mvua kubwa ambayo wakati natafakari ilianza kunyesha kwa upepo mkali ulionifanya nichanganyikiwe, wakati ule familia yote ilikuwa tayari imelala," anasema Lubunda.

Anasema ulianza kuvuma upepo mkali huku na vishindo vikubwa vikisikika, baadaye alisikia kishindo kikubwa kikitokea kwenye nyumba yake ya mbele, lakini kutokana na upepo huo ilikuwa vigumu kuona hali ilivyokuwa nje.
Baadaye alibaini tayari nyumba yake ya mbele ilikuwa imeezuliwa na upepo, alimuamsha mke wake, Hollo Lububu na kwamba baada kuamka alitoka nje kushuhudia.

Lubunda anasema nje alikutana na balaa kwani wakati anatoka hakuwa amevaa viatu, akajikuta miguu yote imezama kwenye barafu iliyokuwa imetanda huku mabonge mengine yakiendelea kudondoka, upepo mkali ukivuma na alifanikiwa kukimbia kuwaamsha watoto wengine na wajukuu.
Wakati akiwaamsha, Lubunda anasema alisikia kishindo kwenye nyumba nyingine hali iliyomlazimu kurudi tena kwa sababu alikuwa akilala binti yake Jane (38), lakini hakufanikiwa kumwokoa kwani alidondokewa na ukuta akafariki dunia.

Licha ya hali hiyo, wakati anakimbia kurudi kwenye nyumba ya binti yake, nje alikutana na jirani yake aliyekuwa amepakata mtoto akamweleza kuwa, kwake nyumba zote zimeanguka na barafu imejaa ndani hivyo alimuomba msaada wa kujihifadhi kwenye banda la gari yake.
Hata hivyo, Lubunda alipoingia nyumba ya binti yake aligundua kwenye chumba cha watoto hawakuwamo, ikabidi aamshe wengine katika chumba kingine waanze kuwatafuta wenzao, ambao waligundulika wawili kati yao tayari walishakufa kwenye udongo huku wengine wawili wakiwa hawajulikani walipo.

Lubunda anasema alikuwa akiwakusanya kwenye banda la gari, wawili hawakuonekana kwa wakati huo huku hali yake ikibadilika kutokana na miguu kufa ganzi kwa sababu ya kukanyaga barafu, wakati mwingine alikuwa akiteleza na kuanguka.
Baadaye watoto walimweleza kuna mwenzao amekimbilia kwenye bwawa baada ya nyumba kubomoka, akidai barafu huyeyuka kwenye maji hivyo mtu anaweza kujikinga kwa kuzama na kuibuka mpaka mvua inapokatika.

Lubunda anasema wakati wote huo sasa kijiji kizima kinapiga yowe ya hatari kila mahali kulikuwa ni kilio na nyumbani kwake sasa wengi walikuwa wameshaamka wengine wakaanza kufukua chumba cha binti yake na kumkuta ameshakufa.

Anasema kuna vijana wengine walimweleza kuwa, kuna mwezao alichukua godoro na kurudi chumbani akawaambia akijifunika godoro hawezi kuathiriwa na mvua hiyo, hivyo waliamua kukimbilia alikokuwa lakini wakakuta tayari amekufa.
Lubunda anasema hali wakati huo ilianza kuwa mbaya kwake, kwani wajukuu zake wengine wawili walikuwa wamekufa wakati wanatoka kujiokoa waliangukiwa na ukuta, hivyo kufikisha idadi ya watu wanne waliopoteza maisha nyumbani kwake.

Wanafamilia ambao walikuwa tayari wameamka zaidi ya 50, mvua ilikuwa imekatika walianza kufuatilia mtoto aliyekimbilia bwawani, lakini hawakufika mbali walimkuta amekufa kwa kuanguka kwenye barafu kabla hajafika bwawani.
Lubunda anaeleza aliishiwa nguvu mithili ya mtu aliyepigwa 'shoti' ya umeme, mwili ulikufa ganzi na kusababisha maumivu ya ndani kifuani hadi tumboni, huku vilio vya vifo vilivyotokana na mvua hiyo vikaanza kusikika kila kona ya kijiji hicho.

Anasema eneo kubwa lilionekana jeupe kutokana na kutapakaa kwa barafu.
Lubunda anasema licha ya umri wake huo, tangu azaliwe hajawahi kukutana na tukio la aina hiyo na kuongeza kuwa hakuna suala lolote linaloweza kufananishwa na mvua hiyo.
Katika familia yake ambayo ni ya kifugaji, anaishi na watu 70 lakini siku hiyo walikuwa zaidi ya 50 aliokoa, watano walipoteza maisha ambao ni binti yake, Jane na wajukuu zake, Lubunda Ng'hwandu (16), Emmanuel Donald (17), Ng'hwelu Nguno (12) na Nguno Nguno.