Washindi 10 wa kubuni wazo la kuanzisha biashara katika shindano lililoanzishwa na kuzinduliwa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, mwezi uliopita, wametangazwa.
Kupatikana kwa washindi hao kunafuatia mchujo wa washiriki takribani 1,680 ambao walituma mawazo yao na kuchujwa na jopo la majaji linaloongozwa na mwenyekiti ambaye pia aliwahi kuwa mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Donath Olomi.
Kati ya washindi hao 10, mmoja alipata tuzo ya Sh. milioni 10 huku wengine tisa wakipewa Sh. milioni moja kila mmoja kutokana na nguvu ya mawazo yao yalivyokuwa.
Mshindi wa milioni 10 kwa mwezi huu ni Fredrick Shayo, kutoka mkoani Kilimanjaro ambaye ni mjasirimali na mfugaji.
Alishinda kwa wazo lake la kuongeza uzalishaji wa kuku wa kienyeji kwa kutotolesha vifaranga kwa kutumia joto la majokofu yaliyoharibika na kuweza kuyasambaza katika maeneo mengine.
Dk. Mengi, aliwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na habari zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye vyombo vya habari kwamba Tanzania haiwezi kuwa na mamilionea.
Aliwataka Watanzania kutokuwa tayari kuwasujudu mamilionea kutoka nje na kuwataka kuwa wabunifu, wanaojiamini na wenye macho ya kuona fursa.
Dk. Mengi aliongeza kuwa Mwenyezi Mungu hakumuumba mtu yeyote kuwa wa pili bali wote nambari moja, huku kila Mtanzania akitakiwa kujiamini, kuwa na macho ya kuona fursa na kuwa na utayari maana bila kufanya hivyo ni vigumu kufanikiwa.
Aliwataka Watanzania kutambua kuwa kuajiriwa siyo njia kuu ya kuzalisha ajira bali ni kujiajiri.
Alishauri kuwapo kwa mifumo kwenye vyuo vikuu ambayo inawaandaa wahitimu kuweza kujiajiri na kuwataka vijana wanapohitimu masomo wasichague kazi ilimradi iwe ya halali na kwamba wanapotaka kuingia kwenye shughuli za kiuchumi kama vile biashara, wasianze na mtaji wa fedha bali wazo bora walilonalo ndiyo mtaji mkubwa na macho yenye kuona fursa.
"Tatizo usianze na mtaji, bali wazo bora. Nguvu yako, wazo lako bora ndiyo mtaji wako mkubwa. Watu wanaona vitu vingi lakini hawazioni fursa. Bila kuwa na macho ya kuona fursa ni vigumu sana kufanikiwa," alisisitiza Dk. Mengi.
Dk. Olomi alitaja mambo muhimu yanayoangaliwa katika kushinda shindano hilo kuwa ni wazo lenye ubunifu, kuhakikisha limebuniwa na mhusika na linaloweza kutekelezeka.
Shayo, alimpongeza Dk. Mengi kwa kuanzisha shindano hilo linalolenga kuwasaidia Watanzania wa ngazi zote ambao wana wazo zuri la kuanzisha biashara, lakini hawana uwezo.
Washiriki ambao ni Watanzania wanatakiwa kutuma mawazo yao kwa ajili ya shindano hilo linaloitwa 3N ambacho ni kifupisho cha 'Nitabuni wazo la biashara, Nitatekeleza, na Nitafanikiwa' kupitia anuani ya twita @regmengi Shindano la Wazo la Biashara.
CHANZO: NIPASHE