Watuhumiwa wa uhujumu uchumi, Reney Petersen (kulia) na Jerry Malekia (katikati), wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jana kujibu shitaka la kuisababishia serikali na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hasara ya Sh. 1,088,640,000 .
Rubani wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), Reney Petersen (28) na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka manne ya uhujumu uchumi.
Pia wanatuhumiwa kuingiza mitambo na kuingilia mawasiliano ya simu za kimataifa bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni moja.
Rubani huyo ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Uholanzi na mwenzake Jerry Diaz (25) walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Janeth Kaluyenda.
Wakili wa Serikali Janeth Kitale alidai kuwa siku isiyofahamika mwaka 2014 washtakiwa huku wakijua ni kosa kisheria, waliingiza nchini mitambo ya kielektoniki ya mawasiliano bila kuwa na leseni ya TCRA.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika jijini Dar es Salaam, washtakiwa walisimika mitambo ya kielektoniki ya mawasiliano bila kupata leseni ya TCRA.
Kitale alidai katika shitaka la tatu, kati ya Machi mwaka 2014 na Januari mwaka 2015 katika jiji la Dar es Salaam, huku wakijua wanafanya makosa, washtakiwa walitumia mitambo hiyo bila leseni ya TCRA.
Ilidaiwa kuwa katika shitaka la nne, kati ya Machi, mwaka 2014 na Januari mwaka huu, washtakiwa waliendesha mitambo hiyo kwa kuingilia mawasiliano na kutumia simu za kimataifa bila leseni ya TCRA.
Ilidaiwa kuwa kati ya Machi mwaka 2014 na Januari mwaka huu, washtakiwa baada ya kuingilia mawasiliano ya simu za kimataifa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 1,088,640,000.
Kutokana na kesi inayowakabili washtakiwa kuwa ya uhujumu uchumi, mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza na kwamba washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.