Meneja Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imewataka wananchi kuacha tabia ya kuweka vyakula vya moto kwenye mifuko ya plastiki, ili kujiepusha na magonjwa yanayoweza kusababishwa na kemikali zilizotumika kutengenezea mifuko hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, Meneja Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza (pichani), alisema kumejengeka utamaduni kwa wananchi hasa katika maeneo ya mijini kutumia mifuko hiyo kuhifadhi vyakula vya moto kama chips na wali bila kujali madhara yake.
"Mifuko ya plastiki imetengenezwa kwa kemikali ambazo zinaweza kumletea madhara mlaji kutokana mwingiliano kati ya chakula na kemikali hizo, ni vyema wananchi wakaelewa kinga ni bora kuliko tiba," alisema Simwanza.
Aidha, aliwataka wananchi na wauzaji wa vyakula kuelewa kuwa, kuna mifuko maalum iliyotengenezwa kwa ajili ya kuwekea na kubeba vyakula vya moto, huku akiwasisitiza mifuko hiyo inafaa kuhifadhi vyakula visivyo vya moto.
Alisema wauzaji wa vyakula wanatakiwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa kuhifadhi na kubebea vyakula ili kuwalinda wateja wao wasipatwe na magonjwa yanayoweza kusababishwa na mifuko hiyo.