Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muunngano wa Tanzania Mohamed Chande Othuman
JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema Kamati ya Maadili ya Majaji imeanza kushughulikia tuhuma za kinidhamu na kimaadili dhidi ya majaji wawili wa Mahakama Kuu, waliotajwa kupata mgawo katika fedha zilizochukuliwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Majaji hao, Aloysius Mujulizi anayedaiwa kupata Sh milioni 40.4 na Profesa Eudes Ruhangisa pia anayedaiwa kupata Sh milioni 400.25 kutoka Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, James Rugemalila.
Jaji Mkuu alisema hayo katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi juzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na ofisi yake dhidi ya tuhuma za kinidhamu na kimaadili, zinazowakabili majaji hao wawili.
Alisema Kamati ya Maadili ya Majaji ilianza kazi yake Januari 26, 2015 na inaundwa na jopo la majaji saba, ambapo wanne ni kutoka Mahakama ya Rufaa na watatu wa Mahakama Kuu. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Jaji Mbarouk Salim Mbarouk.
Wajumbe ni majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Jaji Salum Massati, Jaji Katherine Oriyo na Jaji Bethuel Mmilla. Wengine ni majaji watatu wa Mahakama Kuu, ambao ni Jaji Augustine Mwarija, Jaji Aisha Nyerere na Jaji Imani Aboud.
Jaji Mkuu aliwasihi wananchi kuvuta subira wakati suala hilo linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, zinahusiana na tuhuma hizo dhidi ya majaji hao.
Alifafanua kwamba suala la kumwondoa kazini Jaji kwa tuhuma za kinidhamu au kimaadili au mwenendo mbaya, lina awamu tatu ambapo kuanza kazi kwa tume hiyo ni awamu ya kwanza.
Alisema kamati hiyo itafanya kazi yake ya upelelezi na uchunguzi wa awali na kisha ikiridhika kwamba tuhuma hizo zina uzito, basi itapeleka suala hilo kwenye Tume ya Utumishi wa Mahakama na hatua ya mwisho katika suala kama hili ni kufikishwa kwenye Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba.
Alipoulizwa juu ya shauku ya wananchi kutaka kufahamu muda unaoweza kutumika hadi kufikia tamati ya suala hilo, Jaji Mkuu alisema:'' Kwenye kushughulikia suala hili Kamati ya Maadili ya Majaji na Tume ya Utumishi wa Mahakama zitafanya kazi zake kwa wakati.
''Lakini haziwezi kuharakisha kwa kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria. Kufanya hivyo kunaweza kubatilisha mwenendo mzima na hata maamuzi yao iwapo yatapingwa mahakamani,'' alifafanua Jaji Mkuu.
Aliongeza ''ni vyema tukangojea matokea ya kazi hii, ambayo inatakiwa ifanyike sio tu kwa wakati, bali pia kwa weledi na umakini ili kila mmoja wetu aridhike kuwa haki imetendeka na katiba, sheria na taratibu zimezingatiwa''.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani alipoulizwa juu ya kuundwa kwa kamati hiyo ya Maadili ya Majaji, kuchunguza tuhuma hizo, alisema hatua hiyo ni muhimu na haiwezi kupuuzwa pindi majaji wanapotuhumiwa.
''Tuhuma kwa Jaji au Idara ya Mahakama ni lazima ichukuliwe kwa uzito mkubwa sana ili tuhuma hiyo au hizo zisije zikaanza kuleta doa kwa usafi wa Mahakama kwani Mahakama ni kioo cha jamii na kimbilio la wote wanaotaka haki", alisema.
Alisema ni vizuri wananchi wakaambiwa kwa uwazi juu ya hatua zinazochukuliwa kuhusu suala hili ili kuwaondoa wasiwasi na kwamba linaweza kuchukua muda hadi kufikia mwisho wake.
Alitoa mfano kwamba yeye alikuwa mjumbe katika Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba mwaka 1993, kushughulikia tuhuma dhidi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu wakati huo, John Mwakipesile dhidi ya tuhuma za mwenendo wake wa kikazi. ''Ilituchukua mwaka mzima kukamilisha kazi hiyo na hatimaye kutoa mapendekezo yetu kwa Rais.
Wananchi wasilitazame hili kwamba litashughulikiwa haraka haraka na kumalizika bali litachukua muda,'' alisema. Hatua hiyo dhidi ya majaji hao ni utekelezaji wa Azimio la Tano, kati ya manane ya Bunge kwa Serikali, juu ya sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, lililogubikwa na ukiukwaji wa taratibu na sheria juu ya matumizi ya fedha hizo.
Maazimio hayo nane yalitolewa katika kikao kilichopita cha Bunge. Azimio hilo la Tano lilisema: "Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania".
Akihutubia Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alisema "Azimio hili nimelipokea, tumelijadili. Hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo.
Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge.
Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo.
Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa". Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni IPTL.
Kabla ya hapo, TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Tayari Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ameondolewa katika nafasi hiyo kwa kuwekewa fedha katika akaunti yake Sh bilioni 1.6 za mgao wa fedha za Tegeta Escrow.
Waziri mwingine aliyejiuzulu kwa sakata hilo ni wa Nishati na Madini, Profesa Sospetor Muhongo. Amejiuzulu kwa madai ya kutoshughulikia ipasavyo suala hilo.
Kufuatia sakata hilo, pia maofisa kadhaa wa BoT, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wengine kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za fedha za akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
Zaidi ya Sh bilioni 300 zinasadikiwa kuchukuliwa kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow kwa njia zisizo halali.