Saturday, February 07, 2015

Kafulila Akwama Kufufua Sakata la ESCROW Bungeni....Asema Bunge Limewanyima Watanzania Haki Yao ya Msingi



Kafulila Akwama Kufufua Sakata la ESCROW Bungeni....Asema Bunge Limewanyima Watanzania Haki Yao ya Msingi
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) ameshindwa kuwasilisha hoja binafsi, kuitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kuhusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa katika sakata la iliyokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow.

Lengo la hoja hiyo kwa mujibu wa madai ya Kafulila, ilikuwa kuwezesha Bunge, kufanya uamuzi mwingine wa alichoita ni uchunguzi mpana na wa kina. 
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Bunge kwenda kwa mbunge huyo, ambayo Paparazi imepata nakala yake jana, Bunge limezuia hatua hiyo ya Kafulila, kwa sababu ilikuwa inakiuka Kanuni za Bunge.
Utaratibu uliowekwa na kanuni ya 54 (4) ya Kanuni za Bunge toleo la 2013, umekataza hoja  iliyokwishaamuliwa na Bunge,  isijadiliwe ndani ya miezi 12 isipokuwa kama ni hoja ya kutaka uamuzi huo wa Bunge uliokwishafanyika ubadilishwe.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na Pius Mboya, kwa niaba ya Katibu wa Bunge, imeeleza kwa kuwa hoja ya Kafulila haikusudii kutaka uamuzi huo ubadilishwe, haikubaliki kikanuni.
Barua hiyo ilieleza kuwa suala hilo lilijadiliwa na kuhitimishwa na Bunge katika mkutano wa 16 na 17 na kutolewa maazimio yanayotakiwa kutekelezwa na serikali, ikiwa ni pamoja na Takukuru.
"Tunapenda kukujulisha pia kwamba hakuna ibara yoyote ya Katiba wala kifungu chochote cha Sheria, kinacholipa Bunge madaraka ya kuitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti yoyote ya kiuchunguzi ya Takukuru, ili ijadiliwe bungeni," ilieleza sehemu ya barua hiyo.
  
Awali akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kafulila alisema ripoti iliyojadiliwa awali ilikuwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo inaangalia upungufu wa kisheria, lakini Takukuru wanajadili mpaka kesi za jinai.
Alisema kujadili ripoti ya Takukuru, kungewezesha kuweka wazi watuhumiwa kwa asilimia 70, wakati ile ya CAG ni asilimia 30 tu.
Kafulila alisema baada ya kuzuiwa kutoa hoja yake binafsi, anajadiliana na wanasheria wake kuangalia taratibu za kikanuni ndani ya mamlaka ya Bunge, ili kupata ushauri nini cha kufanya.
Suala hilo la utoaji wa fedha takribani Sh bilioni 200, kwa iliyokuwa akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT), baada ya kuamuliwa, Serikali, Bunge na Mahakama vilipewa maazimio ya kutekeleza.
Tayari kwa upande wa Serikali, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliondolewa katika nafasi yake, huku aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakijiuzulu.
Baada ya hapo, Mahakama nayo imeshaanza utekelezaji kwa kuchunguza watendaji wake wanaotuhumiwa, huku wenyeviti wa Bunge wawili, Andrew Chenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na William Ngeleja, aliyekuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, wakijiuzulu nafasi zao bungeni.