Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kuwapo kwa baadhi ya watumishi wake wanaojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, hivyo kuchafua sifa ya taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na taasisi zilizofanya utafiti juu ya masuala ya rushwa nchini, baadhi yake zina ukweli.
Dk Hoseah alisema wanapokea utafiti huo kama changamoto na watatumia sheria, kanuni na taratibu kuwapa adhabu watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
"Takukuru siyo malaika, iwapo nitasema hakuna kabisa rushwa ndani ya taasisi hii nitakuwa ninajidanganya kwani hili tatizo lipo sehemu zote, inawezekana maofisa wasio waadilifu wanapokea rushwa lakini ninawahakikishia kwamba tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika," alisema Dk Hoseah na kuongeza:
"Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha Takukuru inaboreshwa, ndiyo maana bado sielewi kwanini kuna baadhi ya watumishi wanalalamikiwa kujihusisha na ulaji rushwa, wanalipwa vizuri na kuna mazingira mazuri ya kufanya kazi. Nitafanya jitihada kuondoa changamoto hizi."
Pia, alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na matapeli wanaojitangaza kwamba wao ni maofisa wa Takukuru, hivyo kuomba rushwa kwa baadhi ya maofisa wa Serikali na watu wengine ambao wanabainika kufanya makosa yanayohusiana na ubadhirifu mbalimbali.
Dk Hoseah alisema ili kupambana na rushwa lazima Serikali iwe na uongozi bora na imara, ambao utasaidia kuweka mipango thabiti kwa maendeleo ya wananchi, kufanya mambo kwa uwazi, kuwajibika kwa umma, kuwashirikisha watu katika mipango mbalimbali na kusimamia utawala wa kisheria.