Kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, imesema ndani ya miaka miwili, itasitisha shughuli za uchimbaji na uzalishaji madini hayo, kutokana na soko kuzidi kushuka.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Filbert Rweyemamu alisema hayo juzi katika kikao cha pamoja baina ya mgodi na wajumbe wa Kamati ya Kijiji cha Mwime, iliyoundwa na uongozi wa mtaa wa Mwime kwa ajili ya kusainiana mkataba wa shughuli za maendeleo.
Rweyemamu alisema shughuli za uzalishaji na uendeshaji ni tofauti na mauzo, hivyo kampuni inazidi kutumia gharama kubwa za uendeshaji.
"Kutokana na mgodi kusitisha shughuli za uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo; siyo kwamba dhahabu zimeisha dhahabu ni nyingi mno, isipokuwa tunashindwa kumudu gharama za uzalishaji wilaya ya Kahama ina dhahabu tangu hatujaingia, makampuni mengi yalichimba na kuondoka na sisi tunaondoka", alisema meneja huyo.
Bei ya dhahabu kwa mwaka 2014, imekuwa chini ya dola 1,300 kwa ounce moja kwa muda mrefu. Kufikia Novemba, bei ilikuwa 1,129 kwa ounce moja, hali ambayo imeleta mtikisiko wa uendeshaji wa kampuni za uchimbaji wa dhahabu.
Katika kikao hicho ambacho madhumuni yake ilikuwa ni usainishwaji wa rasimu ya mkataba wa shughuli za maendeleo baina ya Kampuni ya Acacia na Serikali ya Kijiji cha Mwime, kilicho jirani na mgodi, shughuli hiyo ilishindikana kufanyika.
Baada ya kujadili upya, walibaini baadhi ya miradi ya vyoo vitano vinavyogharimu Sh milioni 51 na visima vitano vinavyogharimu Sh milioni 140, havikuwemo katika rasimu hiyo, hali iliyopingwa na Meneja wa mgodi.
Katika mkutano huo Meneja Mkuu wa mgodi huo , Rweyemamu aliwaeleza wajumbe wa Kamati kwamba hawawezi kuanza kuijadili rasimu hiyo kwa kuwa wao kama mgodi, rasimu hiyo waliipeleka kwa Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji wa Kahama na kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mji huo, Felix Kimaryo.
Alisema ni muda mrefu tangu wairudishe rasimu hiyo kwa Ofisa Mtendaji ili Kamati ijadili, kama kuna upungufu wawasiliane na uongozi wa mgodi.
"Ndugu wajumbe wa Kamati hii ni kwamba mkutano huu ulikuwa ni wa kusaini rasimu hii ya mkataba, sasa naona mnasema rasimu hii vyoo na visima havimo, sisi kama mgodi tumekuja kusaini siyo kujadili tena, kazi hiyo tuliwaachia nyie maana sisi rasimu hiyo tuliipeleka kwa Mwanasheria wa Halmashauri na ikapitishwa na Mkurugenzi wa Mji,"alisema Meneja Mkuu huyo.
Alisema, "Mnataka visima gani? Maana tayari tumechimba visima vitano kwa kata nzima ya Mwendakulima vyenye thamani ya Shilingi milioni 140 , tumejenga vyoo katika shule za msingi Mwime thamani vya Sh milioni 51, tumeweza kujenga zahanati kijiji cha Mwime ikiwa lengo la mgodi ni kuweka mahusiano mazuri kwa wananchi wanaozunguka mgodi," alisema.
Rweyemamu alisema kuwa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wake wa Buzwagi, iliweka vipaumbele katika mambo mbalimbali ya maendeleo kwenye mtaa huo, lakini viongozi ndiyo wanakwamisha.
Aliwataka viongozi kujipanga upya huku wakiwa wameweka upungufu wote na wao kama mgodi, watakubali kusaini makubaliano hayo.
Mmoja wa wajumbe wa rasimu ya mkataba huo, Mayala Makoye alieleza kwamba wananchi wa mtaa wa Mwime, wanashindwa kufaidika na matunda ya mgodi huo, kutokana na uongozi wa kijiji hicho kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi, hali inayosababisha wauchukie mgodi na kutamani ufungwe haraka.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mwime, George Kingi, alijitetea kuwa alishirikisha wajumbe 25 na wakakubaliana kuita uongozi wa mgodi, wasaini makubaliano ya rasimu hiyo ya mkataba.