Mkazi wa Rumala wilayani Ilemela, Erick Godwin (21) amekiri kukutwa na fedha bandia ambazo kama zingekuwa halisi zingekuwa na thamani ya Sh70,000, lakini akadai hakuwa anafahamu lolote.
Akijitetea mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana jana, mshtakiwa alidai kuwa aliagizwa na mtu kwenda kutuma fedha hizo kupitia kwa wakala wa M-Pesa, Neema Shuku, maeneo ya Ilwaganzala wilayani Ilemela.
Mshtakiwa alidai alikuwa aingize fedha hizo kwenye simu yake na kwamba, akiwa kwa wakala huyo ghafla alianza kumshambulia.
Shahidi wa kwanza, ambaye ni Shuku, alidai mshtakiwa alikwenda dukani kwake akihitaji huduma ya M-Pesa, alipozipokea fedha hizo alibaini ni bandia.
Shuku alidai mshtakiwa alishambuliwa na baadhi ya watu waliokusanyika, baadaye alitoa taarifa Kituo cha Polisi Kirumba na askari walifika na kumchukua kumpeleka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza kuhakiki fedha hizo.
Alidai baada ya kuhakikiwa ilibainika noti hizo ni bandia, hivyo mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kortini.
Naye mpelelezi kutoka Kituo cha Polisi cha Kirumba, Koplo Saidi alidai baada ya kumkamata na kumhoji, mshtakiwa aliwaeleza kuwa alitumwa na kuzichanganya na fedha zake na hakuwa akitambua iwapo ni bandia.
Koplo Saidi alidai polisi walipomtaka kumtafuta aliyemtuma hakupatikana.
Hakimu Cresencia Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 2 itakapoendelea kusikilizwa tena mahakamani hapo.
MWANANCHI.