KAMATI ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), imekiri kuwa hadi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ipo, lakini pamoja na kusainiwa na Rais bado haijaanza kutekelezwa jambo linalosababisha misamaha ya kodi izidi kupaa.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Ikulu kushangazwa na kamati hiyo kuendelea kulalamikia misamaha ya kodi, wakati wameshindwa kupitisha muswada wa Sheria utakaosaidia kufuta misamaha ya kodi nchini.
"Si kweli kwamba hatujapitisha sheria, Mkurugenzi wa Ikulu aangalie taarifa zake vizuri, Sheria hii tayari imepitishwa ila mpaka sasa haijatekelezwa na ndio maana madhara ya misamaha ya kodi inazidi kuendelea," alisisitiza Zitto.
Alisema baada ya kupokea taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu kuzidi kupanda kwa misamaha ya kodi ambayo imefikia kiasi cha Sh trilioni 1.82 kwa mwaka wa fedha 2013/2014, kamati hiyo ilimuagiza Waziri wa Fedha kuitangaza Sheria hiyo kwenye gazeti la Serikali ili iweze kutekelezwa.
Alisema pamoja na kwamba Sheria hiyo awali ilikuwa na mapendekezo makubwa ambayo yangewezesha tatizo la misamaha ya kodi nchini kuwa historia, ilipopitiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, mapendekezo hayo yalipunguzwa ili kuwezesha misamaha ya kodi kuzidi kuendelea nchini.
"Hili ndio tatizo kubwa tulilonalo sasa, sisi Kamati ya PAC tunataka na tunapendekeza na kila siku tunasisitiza juu ya kuondolewa kwa misamaha hii ya kodi, lakini wenzetu wa Kamati ya Bajeti hawataki wanataka misamaha ya kodi iendelee," alisema.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Sheria hiyo ya VAT iliyotakiwa kutekelezwa tangu Januari mwaka huu, ina wigo mkubwa wa kupunguza tatizo hilo la misamaha ya kodi endapo haitaendelea kukaliwa na Serikali.
Aidha, Zitto alimwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) awasiliane na Serikali ili kubaini chanzo na sababu zinazofanya sheria hiyo hadi sasa haitangazwi kwenye gazeti la Serikali na kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria.