Friday, January 16, 2015

Wateja StarTimes kununua king’amuzi kwa shilingi 4000


Wateja StarTimes kununua king'amuzi kwa shilingi 4000
Meneja Mauzo wa StarTimes Tanzania, David Kisaka (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa bei mpya ya king'amuzi kitakakochouzwa kwa shilingi 4000 sambamba na kifurushi kipya cha NYOTA cha malipo ya 4000 kwa mwezi, kulia pamoja naye ni Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo, Jacky Yu. Bei hiyo mpya ya king'amuzi na kifurushi itamfanya mteja afurahie chaneli zisizopungua 16 ikiwa 9 ni za kimataifa na 7 za nyumbani kwa muda wa miezi saba na nusu.
Baadhi ya wateja waliokuwepo kwenye uzinduzi wa bei mpya ya king'amuzi kitakakochouzwa kwa shilingi 4000 sambamba na kifurushi kipya cha NYOTA cha malipo ya 4000 kwa mwezi. Bei hiyo mpya ya king'amuzi na kifurushi itamfanya mteja afurahie chaneli zisizopungua 16 ikiwa 9 ni za kimataifa na 7 za nyumbani kwa muda wa miezi saba na nusu. Uzinduzi huo ulifanyika katika duka la kampuni hiyo lililopo ofisi za TBC1, Mikocheni-Bamaga jijini Dar es Salaam.

Kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora na nafuu za matangazo ya dijitali, StarTimes imekuja na kifurushi kipya na bei mpya ya king'amuzi kwa shilingi 4000/- tu gharama ambayo ni ya chini kabisa kutowahi kutokea nchini.

Akizungumzia juu ya huduma hii mpya Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Star Media Tanzania ambao ni wauzaji wa ving'amuzi vya StarTimes nchini, Bw. Jacky Yu amebainisha kuwa uzinduzi huu ni sehemu ya kutimiza ahadi kwa watanzania kwamba watakuwa wakitoa huduma bora na kwa bei nafuu ambayo kila mtu ataweza kuimudu.

"Leo tunayo furaha kubwa kabisa kuwatangazia umma wa watanzania kwamba StarTimes imeshusha bei ya king'amuzi chake mpaka kufikia shilingi 4000 na kuzindua kifurushi kipya na cha bei ya chini kinachokwenda kwa jina la NYOTA ambacho kitapatikana kwa malipo ya shilingi 4000 kila mwezi."

"Kifurushi hiki kipya cha NYOTA kina jumla ya chaneli zisizopungua 16, saba ni za nyumbani na 9 ni za kimataifa ambazo ni Star Swahili, Bollywood Swahili, E-Star, Star Music, Kungfu 1, Child Smile, TBN, TV Imani na CCTV News. Ili mteja aweze kuunganishwa na kifurushi hiki itabidi aambatanishe na malipo ya awali ya shilingi 30,000 na kuweza kufaidi kwa muda wa miezi saba na nusu." Alifafanua zaidi Bw. Yu

Aliendelea kwa kusema kuwa, baada ya muda wa ofa iliyotolewa kwa wateja wa kifurushi kipya cha NYOTA kuisha, mteja ataamua kama anaendelea  na kifurushi hiki cha kulipia shilingi 4000 kila mwezi au kutazama vingine vya kawaida. Ili mteja kurudishwa katika vifurushi vya kawaida ambavyo vitamruhusu kutazama chaneli za bure za nyumbani na kulipia vifurushi vilivyopo basi itambidi afuate njia ya kawaida ya kujiunga ambayo ni rahisi kwa kupiga *150*63# na kufuata maelekezo au atembelee ofisi zetu na za mawakala.

"Madhumuni makubwa ya bei hii mpya ya king'amuzi na kifurushi cha NYOTA ni kumtaka kila mtanzania hata Yule wa kipato cha chini aweze kupata matangazo ya dijitali. Tuna imani kubwa kwamba kifurushi hiki kipya kitakidhi mahitaji ya wateja wetu wote ambao wanapenda huduma zetu lakini hushindwa kulipia gharama za vifurushi vilivyopo." Alisema Bw. Yu na kumalizia, "Siku zote StarTimes tutaendelea na dhamira yetu ya kutoa huduma za uhakika na kwa bei nafuu ili kumfikia kila mteja. Tunaimani matangazo ya dijitali ni fursa ambayo kila mtanzania lazima anufaike nayo."

Naye kwa upande wake Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Bw. David Kisaka aliongezea kwa kusema, "kifurushi hiki kipya kimeongezewa katika vifurushi vyetu vilivyopo, hivyo basi kuanzia leo hii tutakuwa na jumla ya vifurushi vinne ambavyo ni NYOTA, Mambo, Uhuru na Kili. Tulichoongezea ni unafuu na kuwajali wateja wetu kwani tunatofautiana kwa hali za kiuchumi na tunafahamu kwamba watanzania wengi ambao ni wateja wanavipato vya kawaida. Tunaamini kwa kifurushi hiki kipya cha NYOTA sasa tutawafikia watanzania wote na kuwawezesha kufurahia matangazo ya dijitali."

"Ningependa kutoa wito kwa wateja wetu kutembelea maduka yetu na ya mawakala wetu popote yalipo ili kuweza kuhudumiwa au kupiga namba ya huduma ya wateja ambayo ni 0764 700 800 ili kupata maelezo na ufafanuzi zaidi. Na pia ningependa kuwatoa hofu huduma hii ni endelevu kwani ni mwanzo tu wa maboresho ya huduma zetu kwani kuna mabo mazuri lukuki yapo njiani yanakuja. Na kwa wale wasio wateja wetu basi huu ndio muda muafaka kwa wao kuunganishwa na huduma zetu, wameshapitwa na mengi lakini hili si la kuliacha lipite hivi hivi." Alihitimisha Bw. Kisaka