Walimu Jiji la Mbeya, wakiwa wamezuiwa na FFU ili wasiendelee kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya.
WALIMU wa shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wapatao 113, juzi waliandamana kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kwa ajili ya kudai haki zao mbalimbali.
Maandamano hayo ya amani, yalianzia katika ofisi kuu ya Jengo la CWT Mkoa wa Mbeya majira ya saa 5;27 asubuhi, kabla hayajazuiwa na kikosi cha askari wa kutuliza ghasia mkoani hapa saa 5;33 mpaka saa 5;39 na kuwaomba warejee ofisini kwao kutokana na hali ya vurugu iliyokuwa imelizingira Jiji hilo jana.
"Tunawaomba mrudi ofisini kwenu na sisi tutaenda kumleta Mkurugenzi wa Jiji, kwasababu hata mkijaribu kwenda muda huu hamtaweza kuonana naye, ulinzi umeimarishwa sana kutokana na mgomo wa wafanyabiashara wa soko la Soweto ambao wamegoma na wanataka kuandamana" alisikika mmoja wa askari mwenye nyota tatu, akiwasihi walimu hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari, walimu hao walisema kuwa, walifikia uamuzi wa kwenda kumuona mwajiri wao kutokana na madai mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara yao tangu mwaka 2007.
"Mwalimu unaingia darasani ukiwa na mawazo ya fedha zako huku ukiangalia dawati la mwanafunzi limechoka. Serikali inajisikia raha kuona mwalimu anaenda na biashara ya ubuyu shuleni! Mimi nadai zaidi ya Milioni Nne tangu mwaka 2007 sijalipwa na fedha tunaambiwa zimekuja zinafanya kazi zingine"alisema Mwalimu Stella Robson.
Mwalimu Lucas Mahenge, ambaye ni mlemavu wa macho, alisema kuwa yeye madai yake ni suala la kupandishwa madaraja bila kupandishwa mshahara, hali ambayo alisema inamkatisha tamaa na serikali isifikie mahala ikawafikirisha walimu kuanza kuwafundisha watoto kuwa 2+2=22.
"Serikali kama imeshindwa kutulipa madai yetu, ituambie ili tuweze kumwomba mfanyabiashara, Rwegemalil" alisema Mwalimu Gunza Mwasomola.
Katibu wa Chama cha walimu Jiji la Mbeya, Mwalimu Felix Mnyanyi, alisema kuwa kwa kushirikiana na viongozi wenzake, wamefuatilia kwa muda mrefu madai hayo na kufanya uhakiki lakini utekelezaji wake umekuwa siyo wa kuridhisha.
"Walimu wamefika hapa wakiwa na madai zaidi ya matatu, ambayo ni malimbikizo ya mishahara tangu mwaka 2007, ambapo ni wilaya pekee nchini walimu hawajalipwa, madai ya fedha za likizo, kupanda na kushushwa madaraja baada ya kujiendeleza kitaaluma na walimu wastaafu kutolipwa" alisema Mwalimu Mnyanyi.
Alisema kuwa baada ya kuzuiwa na kuwaelewa askari polisi kuwa wasifike katika ofisi ya mwajiri wao ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, kutokana na hali ilivyokuwa ya utata wa usalama wao na watu wengine, walirejea ofisini hapo na kuendelea kumsubiri mwajiri huyo chini ya ulinzi wa polisi, hali ambayo mpaka majira ya saa saba mchana, walimu waliendelea kuwepo katika ofisi yao na Mkurugenzi hakuweza kufika kwa wakati huo mpaka tunaenda mitamboni.
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza, alikiri kuwepo madai ya walimu katika ofisi yake na kwamba madeni hayo hayatawezwa kumalizwa kwa siku moja kutokana na walimu kutofautiana muda wa kuanza likizo na kumaliza.
Alwaambia walimu kuwa atashughulikia madai yao kwa kushirikiana na uongozi wao wa CWT.