Wednesday, January 21, 2015

TUUNGANE KUMTAFUTA MTOTO PENDO



TUUNGANE KUMTAFUTA MTOTO PENDO A policeman holds up a picture of          missing albino girl Pendo Emmanuelle Nundi
KATIKA vyombo vya habari vya jana hasa magazeti, kulichapishwa picha ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola akionesha picha ya mtoto Pendo Emmanuel (4) ambaye ametekwa na watu wasiojulikana.



Mtoto huyo ambaye alikuwa anaishi na wazazi wake katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba hadi sasa haijulikani aliko au mahali alikofichwa.


Ni kutokana na kutokuwapo kwa taarifa yoyote ya kupatikana kwa mtoto huyo kumeifanya Polisi sasa kuonesha picha yake ili kuwezesha wasamaria wasaidie kupatikana kwa binti huyo.
Polisi imetoa picha hiyo baada ya kushindwa kumpata mtoto huyo ambaye alitekwa usiku wa Desemba 27 mwaka jana akiwa amelala pamoja na wazazi, baada ya watu hao kuvamia nyumba hiyo na kupora mtoto huyo na kutokomea kusikojulikana.
Sasa Polisi imeona njia pekee iliyobaki ya kumwokoa binti huyo ni kuchapisha picha yake na Mlowola ametoa mwito kwa yeyote atakayemwona mtoto huyo atoe taarifa katika kituo cha Polisi ama kwenye ofisi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Pendo ambaye ana ulemavu wa ngozi ni miongoni mwa albino ambao wamenyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili kwa sababu tu ya kuwa ngozi hiyo ambayo baadhi ya watu ambao wanaamini katika ushirikina wanadai kuwa viungo vya walemavu hao vina bahati ya kupata mali.
Mali hiyo inaweza kutumiwa na wachimbaji wa madini, wavuvi wa samaki au wanasiasa mara wanapokuwa kwenye harakati zao za kuwania nafasi ya udiwani, ubunge na urais.
Yaani ni kwamba watu wa namna hiyo wanachohitaji ni albino afe au ateswe na wao wapate wanachokihitaji. Kwa hiyo tamaa ya mali ndio imechangia hadi sasa albino 15 mkoani Mwanza kuuawa tangu mwaka 2008 kutokana na imani za kishirikina.
Idadi hiyo ni sehemu ya idadi ya albino zaidi ya 70 ambao wameshauawa tangu mwaka huo ili kuwafanya wengine watajirike. Hilo la kumteka mtoto ni jipya katika matukio haya ya kuwafanyia ukatili albino, awali tumezoea kusikia nyumba kuvamiwa na mtu kukatwa viungo au kuuawa na kukatwa viungo. Lakini sasa wameona viungo peke yake havitoshi.
Yawezekana sasa wameamua kumchukua mzima ili waweze kupata viungo vingi vya kuuza, yaani kwamba wanataka wapate fedha kwa kuuza kiungo cha binadamu mwenzao.
Hawa watu hawana hofu ya Mungu bali wanaongozwa na matendo ya shetani. Huo utajiri wanaoutaka pia ni wa kishetani na kama ni wanasiasa wanataka wapate madaraka na kiongozi wa namna hiyo kamwe hawezi kuwaongoza watu wake katika kutenda matendo mema.
Ataongoza kishirikina na hatakuwa na moyo wa kujali. Kuna hatua nyingi zimechukuliwa na Serikali kuhakikisha zinazuia mauaji haya ambayo yameshamiri zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini bado wahalifu hao hawataki kuamini kwamba upatikanaji wa mali unatokana na mtu kujituma kufanya kazi kwa bidii.
Licha ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kutoa siku tano, mtoto huyo awe amepatikana, lakini hadi sasa hajapatikana na hakuna taarifa zozote ambazo zitasaidia mtoto Pendo aweze kupatikana.
Kitendo alichofanyiwa mtoto huyo ni cha kinyama kwani hadi sasa hatujui kama yuko hai au tayari ameuawa. Ni vyema polisi waendelee na msako wa nguvu na waliokamatwa pia wawasaidie namna ambavyo mtoto huyo anaweza kupatikana.
Lakini jamii yote na wapenda amani kote nchini tuungane pamoja kumsaka mtoto huyu. Polisi peke yake hawawezi kufanikiwa kumpata bila kupata ushirikiano kutoka kwa jamii. Ni sisi wanajamii ndio tutakaowezesha mtoto Pendo apatikane