Wednesday, January 21, 2015

THOMAS MPONDA: ALBINO ALIYEOKOLEWA NA MUNGU KILA ALIPOTAKA KUUAWA


THOMAS MPONDA: ALBINO ALIYEOKOLEWA NA MUNGU KILA ALIPOTAKA KUUAWA
PICHAHII HAIHUSIANI NA HABARI HUSIKA

Wiki hii katika jitihada za kupambana na waua albino, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, alitangaza kupiga marufuku kazi za ramli na kuundwa kikosi kazi cha kuwanasa watakaokiuka agizo hilo.



Hizo ni habari njema japo hazina jipya kwa sababu albino wameuawa kwa muongo mzima lakini serikali haijafanya kazi kikamilifu kuwalinda na kuwaadhibu wauaji. 

Katika mfululizo wa visa vya unyanyasaji na uuaji  albino ni vyema kusikia wanasemaje  kuhusu maisha yao na jinsi wanavyoishi na 'dunia' isiyo rafiki, pata ukweli huo ndani ya mahojiano  ya Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino mkoani Pwani Thomas Mponda, na  Margaret Malisa, kuhusu vita dhidi ya uhai wa albino.

SWALI : Tupe historia ya maisha yako, mahali  ulipozaliwa na kama una familia.

MPONDA: Nilizaliwa hapa Kibaha Msangani mwaka 1970  nina miaka 45. Kwa asili ni mwenyeji wa Morogoro lakini baba yangu alikuwa seremala na pia mganga wa kienyeji hivyo alikuja kikazi Kibaha na ndipo na mimi nikazaliwa huku. Nimeoa na nina watoto wawili Barack na Glory. 

SWALI: Katika maisha yako umewahi kuwindwa na kushambuliwa na wauaji? 
MPONDA: Nimenusurika katika majaribio mawili ya kuuawa kama ambavyo. 

Majaribio ni mengi lakini nayakumbuka mawili kwa kuwa nilikuwa nimeanza kuwa na akili  lakini ukweli ni kwamba visa vya kuuawa vilianza pale tu nilipozaliwa.

SWALI: Ilikuwaje? Na familia  yako ilipokeaje kuzaliwa kwa albino katika ukoo wenu?

 MPONDA: Kwa kweli kuzaliwa kwangu hakukufurahiwa na hata mtu mmoja kwani baba yangu mzazi  alipopata taarifa alisema yeye hawezi kuzaa mtoto albino mwenye rangi mbili kama 'tetrasaklini' na inasemekana kuwa nilipofikisha siku mbili niliugua na baba akasema kuwa siwezi kuishi.

Alifurahi akisema  ni  kheri nikafa lakini haikuwa mipango ya mungu, nikapona na sasa ninadunda.

Haikushia hapo baba yangu aliamua kumfukuza mama kwa kukataa kuniua mimi hivyo mama akaamua kwenda  nami kuishi kijiji cha Dionzele Bagamoyo kwa ndugu zake. Lakini masahibu hayakuishia hapo baada ya kufika kule nikiwa na miaka minne mama mkubwa na shangazi walimwambia mama aniulie mbali na asiponiua watafanyakazi hiyo.

"Muue huyo kama sivyo sisi tuatamua wenyewe," ni maneno ya  mama yangu anayoambiwa na ndugu zake,  lakini mama yangu alipingana nao na kunitetea. 
Baada ya kuona mama hakubaliani nao waliamua kupanga mbinu nyingine za kuniua siku hiyo ambayo sitoisahau. 

Mama alikwenda kufanya kibarua ili  kupata mahitaji. Mimi bila kujua  huku nyumbani  shangazi na mama mkubwa walisaga chupa na kuziweka kwenye uji wangu  ili nikila nife. 

Lakini bibi yangu mzaa mama alikuwapo japo alikuwa mzee na hawezi kutembea wala kuongea  alishuhudia ile njama iliyokuwa inaendelea na hakuwa na cha kufanya. Kwa hiyo akabaki kama shuhuda aone nitakavyokufa  ili aje amsimulie mama atakaporudi.

Basi  mwandishi, mimi nilikuwa nacheza na watoto wenzangu huko nje, tulipoitwa kula kila mtu alikuwa ana kibakuli chake iwe ni uji, au chochote ingawa kipindi kile tulikuwa tukila ukoko, lakini nina chokumbuka tulikuwa  tunachezea ringi za matairi ya baiskeli zinazotumiwa na Wamasai kwa kuwa tulikuwa tukiishi nao karibu.

Basi nilipopewa kile kibakuli nafsi yangu ikaniambia nisinywe, kwa hiyo sikunywa ule uji nikachukuwa bua langu nikapachika kwenye ringi na kwenda kucheza, kumbe ndiyo nilikuwa napona bila kujua chochote. 

Mama aliporudi bibi alimueleza tukio zima na  wao walipoulizwa walisema ni kweli walitaka kuniua kwani mama kila akiambiwa animalize alikuwa haafiki.
SWALI : Baada ya kunusurika kuna kisa kingine?

MPONDA: Hilo ndilo lilikuwa tukio la kwanza ambalo nilinusurika  kwa rehema za Mungu, lakini tukio jingine lilitokea siku nyingine majira ya mchana ndugu hao waliniita kwa jina langu la nyumbani, "Mponda chite kudisima"…… maana yake Mponda twende kisimani, zamani kule kwetu maji yalikuwa ni shida na ni mbali kwa hiyo kwa watoto wanaweza kutembea walikuwa wanakwenda kuoga huko huko kwani mama akirudi  na mtungi yeye ni wa  maji ya kunywa na kupikia si vinginevyo. 

Siku zote huwa tulikuwa tunakwenda,  lakini siku hiyo waliponiambia nafsi yangu ilikataa  kwa hiyo nikachukuwa kigari changu cha mabua nikakimbia kwenda kucheza kwa majirani.

Kumbe siku ile walipanga kwenda kunitupa kisimani ili nifie majini, sasa jaribio hilo liliposhindikana kwa kuwa walishindwa kunilazimisha kwenda kunitupa kisimani wakamwambia mama mtoto wako ana mashetani makali  kwani kila tunachokipanga kumuua anakigundua na anakataa.

SWALI: Mama mkubwa  na shangazi yako leo wako wapi?
MPONDA: Bahati mbaya wote wawili pamoja na  baba yangu wamefariki muda  mrefu sasa. 

Lakini mama mkubwa hadi anafariki alikuwa akiamini mimi nina majini makali ambayo yanajua mambo mbalimbali yanayopangwa, kwa hiyo kwa kifupi mimi nilitakiwa nisiishi lakini Mungu alininusuru kwa rehema zake.

SWALI: Kwa hiyo unataka kusema mauaji ya albino yalianza tangu zama za mababu na je, kama yalianza  kuna tukio lolote  lililokuwa linamhusu albino au ulilowahi kusikia linalohusiana na mauaji ya albino katika kipindi hicho? 

MPONDA: Ndiyo kuna watoto wa shangazi yangu wawili waliuwawa kwa kuwekwa katika mtungi hadi wakafa, kwa hiyo hata mimi nilinusurika walikusudia kunimaliza, kwa hiyo suala la mauji ya albino yalikuwepo tangu zamani lakini yalifanyika kwa siri. 

Sasa hivi tunashukuru vyombo vya habari vimeibua na kuweka wazi kila mtu akajua na harakati za wadau mbalimbali zikaanza katika kuhakikisha mauaji ya albino yanakoma.

SWALI : Ukiwa  mwenyekiti wa chama maalbino hapa Pwani, hivi karibuni kumekuwepo wimbi la mauaji ya albino katika maeneo kadhaa hapa nchini vipi   Pwani hali ikoje?

MPONDA: Mauaji ya albino kwa mkoa wa Pwani hatujapata lakini majaribio ya mauaji yamekuwepo kwani kuna watoto wanne walinusurika kufa, mmoja alikatwa mguu mwaka jana lakini muuaji hakupatikana hadi sasa. Watuhumiwa hawakupatikana licha ya chama kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuwasaka.