Thursday, January 22, 2015

Spika wa Bunge amesema sio jukumu lake kuwaondoa wenyeviti wa kamati za Bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la Escrow



Spika wa Bunge amesema sio jukumu lake kuwaondoa wenyeviti wa kamati za Bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la Escrow

Spika wa bunge Mh Anna Makinda amesema siyo jukumu lake kuwaondoa wenyeviti wa kamati za bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow isipokuwa wao wenyewe wanatakiwa kutii azimio la bunge namba tatu linalowataka wajiuzulu.
Wakati Mh Makinda akieleza hayo tena kwa kusisitiza kuwa wenyeviti hao tayari wameshajiuzulu baadhi ya kamati ikiwemo ya katiba na sheria ambayo mwenyekiti wake ni Mh William Ngeleja ambaye ni miongoni mwa wabunge wanaotuhumiwa kwenye sakata hilo bado anaendelea na wadhifa huo.
 
Mh Makinda ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kupokea msaada wa vifaa vya Teknohama vilivyotolewa na serikali ya China kupitia balozi wake hapa nchini ambapo amesema vifaa hivyo vitaweza kuokoa zaidi ya bilioni moja ambazo hutumika kuchapisha miswada mbalimbali na taarifa nyingine za bunge badala yake sasa wabunge watakuwa wanatumiwa moja kwa moja kwenye mtandao.
 
Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya dola za kimarekani laki moja balozi wa china hapa nchini Lu Youqing amesema vifaa hivyo ni ahadi aliyoitoa rais wa China wakati wa ziara yake hapa nchini ambapo alimwahidi spika wa bunge Mh Makinda na kuongeza kuwa china imewekeza zaidi ya dola bilioni 3.1 hasa sekta ya kilimo na viwanda na kwamba kuna kampuni zaidi ya 500 zinazomilikiwa na wachina ambazo zimetoa ajira kwa watanzania laki moja.