Thursday, January 22, 2015

Basi la Taqwa lanaswa na shehena ya magendo, likitokea harare kwenda Dar



Basi la Taqwa lanaswa na shehena ya magendo, likitokea harare kwenda Dar


Abiria zaidi ya 60 ambao walikuwa wakisafiri kutoka harare nchini Zimbabwe kwenda jijini Dar es salaam wamekwama jijini mbeya kwa zaidi ya saa sita,baada ya basi lenye namba za usajili T776 CRN mali ya kampuni ya TAQWA walilokuwa wakisafiria kukamatwa likiwa limebeba bidhaa mbalimbali za magendo zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 39.
Msako wa kushtukiza katika vyombo vya usafiri ambao umefanywa na mamlaka ya chakula na Dawa, TFDA, na mamlaka ya mapato tanzania, TRA, kwa kushirikiana na jeshi la polisi ndio ambao umelinasa basi hilo likiwa limesheheni bidhaa za aina mbalimbali yakiwemo maziwa ya watoto aina yaLACTOGEN ambayo hayajasajiliwa nchini na hivyo kuhatarisha afya na maisha ya watanzania.
 
Afisa wa forodha wa TRA mbeya, Edward Male, akatumia fursa hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara na watu wengine wenye tabia ya kufanya biashara ya magendo.
 
Baada ya basi hilo kushikiliwa kwa muda mrefu, abiria wake wengi wao wakiwa ni raia wa nchi za zambia na zimbabwe ambao walionesha kuwa wachovu wa safari  na wenye njaa, nao wakaanza kutoa kilio chao, wakihitaji msaada ili waendelee na safari yao.
 
Malalamiko hayo yakatua kwenye sikio la mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu SUMATRA, ambao ikawabidi kuingilia kati na kuhakikisha abiria wanaendelea na safari yao.