Na Greyson Mwase, Maswa.
Meneja Utaalamu Elekezi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Gissima Nyamohanga amesema kuwa serikali imetumia shilingi bilioni 881 katika mradi wa kusambaza umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
Nyamohanga aliyasema hayo kwenye sherehe za uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA uliofanyika katika kata ya Shishiyu wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Alisema kuwa Mradi wa REA Awamu ya Pili utaiwezesha idadi ya vijiji vilivyounganishwa na umeme 3734 kati ya vijiji 15,180 ambayo ni asilimia 24.6 kufikia vijiji 5,234 ambayo ni asilimia 34.5 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa mradi wa REA Awamu ya Pili wa miaka miwili ulioanza mwaka 2013, lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapatiwa umeme hivyo kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Akielezea mchango wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA katika kuboresha maisha ya wananchi Nyamohanga alisema kuwa awali wananchi wote walikuwa wakilipa shilingi 467,000 kama gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ilikuwa ni kubwa na kupelekea wananchi wachache wenye uwezo kuwa na nishati ya umeme huku ikiacha kundi kubwa la wasio na uwezo kuishi gizani.
Alisema kuwa katika Awamu ya Kwanza ya REA gharama za uunganishaji wa umeme zilishuka kutoka shilingi 467,000 hadi shilingi 177,000 na kuongeza kuwa katika kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuunganishiwa umeme Serikali iliamua kubeba gharama zote kupitia REA Awamu ya Pili na wananchi kutakiwa kuchangia shilingi 27,000 tu kama kodi ya ongezeko (VAT)
Alieleza kuwa mara baada ya kumalizika kwa Awamu ya Pili ya REA, viongozi wataainisha vijiji ambavyo havijapata umeme REA Awamu ya Pili, ambapo vitajumuishwa katika mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Nyamohanga alieleza michango mingine kuwa ni kufungua fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana wa kitanzania, ufaulu kuongozeka kwa shule za sekondari na kuboreshwa kwa huduma za afya.
"Kwa mfano kwa shughuli za kiuchumi bei ya kusaga debe la mahindi ilikuwa ni shilingi 1,000 itashuka hadi shilingi 500 kutokana na kwamba mashine za kusaga zitakuwa zinatumia umeme badala ya dizeli kama zamani," alisema Nyamohanga
Wakati huohuoMeneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Kanda ya Ziwa Mhandisi Joyce Ngahyoma akielezea jinsi ya kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi wa vijiji vilivyopitiwa na mradi wa REA Awamu ya Pili alisema kuwa wananchi wanaoishi mita 30 karibu na miundombinu ya umeme wataunganishiwa kwa shilingi 27,000 na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo kwa kuboresha makazi yao.
Alisema kwa wananchi wenye nyumba zenye vyumba viwili na vioski hawahitaji kufunga mfumo wa umeme kwenye nyumba zao (wiring) badala yake watashauriwa kununua kifaa maalumu kijulikanacho kama "UMETA" (Umeme Tayari) kinachoweza kutumika kama mfumo kwa kuwa na uwezo wa kuunganisha taa mbili na vifaa vingine kama vile jiko, friji na pasi.
Aliendelea kusema kuwa kifaa hicho kinachouzwa kwa gharama ya shilingi 37,000 kitakuwa ni mali ya mteja na endapo atahama makazi basi atakuwa huru kuhama pamoja na kifaa chake.