Sunday, January 04, 2015

RAIS JK AIDHINISHA WAUAJI WA ALBINO WANYONGWE



RAIS JK AIDHINISHA WAUAJI WA ALBINO WANYONGWE


Chama cha Albino Tanzania  (Tas) kimemuomba Rais Jakaya Kikwete, aidhinishe utekelezwaji wa hukumu ya kuwanyonga hadi kufa, wafungwa waliopatikana na hatia ya kuwaua albino.



Akizungumza kabla ya kuhitimisha Mkutano Mkuu wa Kamati Kuu ya TAS, wiki hii mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Tas – Taifa, Ernest Kimaya, alisema ombi hilo ni moja ya maazimio waliyoyafikia na yasipotekelezwa ndani ya miezi mitatu, watapeleka maombi maalumu Umoja wa Mataifa (UN).

Tangu mauaji ya albino yalipoanza karibu miaka 15 sasa  wafungwa watano wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa  lakini hakuna aliyetiwa  kitanzi.

Wengi wawauaji hao wapo kwenye magereza ya kanda ya Ziwa na miongoni mwao  yupo mganga wa jadi.

Kimaya alitoa fursa kwa viongozi wa Tas wa mikoa ya Mwanza, Pwani, Kagera, Ruvuma na Kilimanjaro kuelezea hali inayowakabili kwenye maeneo yao na kusema kuwa hawaridhishwi na hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya ukatili na mauaji yanayoendelea nchini.

"Serikali isipotekeleza maazimio tunayotoa leo kwa wakati tulioutoa, tutaomba UN iunde tume itakayofanya kazi bila kuingiliwa na chombo chochote cha hapa nchini, kuchunguza kiini na wanaohusika na vitendo hivi na pia iwashitaki na hukumu zitolewe", alieleza Kimaya.

Alitaja azimio lingine kuwa ni serikali kuhakikisha inampata mtoto ,Pendo Emmanuel, aliyeporwa kwa wazazi wake, nyumbani kwao Kwimba mkoani Mwanza, wiki iliyopita. Alisema vinginevyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, ajiuzulu.

Alisema polisi wana uwezo wa kutekeleza kwa ukamilifu azimio hilo, akitoa mfano wa kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Ballow.

Alieleza kuwa  muda mfupi baada ya tukio hilo, vifaa vyote hata vilivyokuwa vimefichwa kwenye chemba ya choo vilipatikana na watuhumiwa wote walikamatwa.

Katibu wa Tas  mkoani Pwani, Aichi Ngule, alisema ingawa Rais Kikwete aliwahi kukaririwa akisema hatasaini hukumu ya aina hiyo, hali ilinavyoendelea hana budi kutekeleza jukumu hilo la kikatiba.

"Katiba inatupa haki ya kuishi, mwenye jukumu la kuilinda na kusimamia utekelezwaji wake ni Rais, kwahiyo tunaamini hawezi kuvunja Katiba na kukiuka kiapo chake," alieleza Aichi.

Alisema wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo, watu 67 walikuwa wameuawa lakini sasa wameongezeka hadi zaidi ya 95, idadi aliyosema ni ambayo imetangazwa.

Kwa mujibu wa Tasa wanasiasa wanahusika kuwaua albino, Katibu wa chama hicho mkoani Kagera, Ignas Lugemarila, alisema kuna viashiria kuwa walio nyuma ya mauaji na ukatili huo, ni wanasiasa.

Alitaja viashiria hivyo kuwa ni pamoja na kutotekelezwa kwa ukamilifu hatua za kubainisha na kuadhibu watuhumiwa wa matukio hayo, kutokana na vikwazo kutoka kwa viongozi wa nganzi tofauti.

"Kila unapowadia wakati wa uchaguzi, tunashuhudia matukio ya kukatwa viungo, kuuawa na sasa kuporwa mtu mzima mzima, tena wanaokamatwa wakifikishwa polisi, wanadhaminiwa na viongozi," alibainisha.

Alisema uchaguzi wa mwaka 2010 alivamiwa, mlango wa nyumba yake, ukavunjwa, aliokolewa na majirani ambao walimkamata mshukiwa wa tukio hilo na kumfikisha polisi kabla hajadhaminiwa na Mtendaji wa Kijiji.

Alisisitiza kuwa kipindi hiki cha uchaguzi, mwenzao mmoja mkoani Ruvuma ameshakatwa vidole vyote vya kiganja cha mkono wa kulia na pia mtoto, mdogo wilayani Kwimba ametoweka mikononi mwa wazazi wake.

Kiongozi mwingine wa Tas wa Kilimanjaro, Febronia Minja, alielezea kuwa Julai 20 mwaka huu, alivamiwa na mtuhumiwa  (jina linahifadhiwa) aliyetamba kuwa alikusudia kukata viungo vyake.

Alisema baada ya kufikishwa polisi alidhaminiwa na Diwani (jina linahifadhiwa) na kwamba Septemba mwaka jana, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani au kulipa faini ya shilingi 420,000 ambazo  alizilipa.

CHANZO: NIPASHE