JESHI la polisi nchini Kenya limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa Shule ya Msingi Lang'ata iliyopo jijini Nairobi walioandamana kupinga kitendo cha kunyang'anywa uwanja wao wa michezo uliouzwa kwa mwekezaji binafsi.
Polisi hao wakiwa na mbwa waliwatawanya wanafunzi hao, baadhi yao wakisemekana kuwa watoto wenye umri wa miaka sita baada ya kuangusha ukuta mpya uliojengwa kutenga shule yao na Uwanja.
Wanafunzi hao walikuwa wamerejea shuleni Lang'ata baada ya mgomo wa wiki mbili wa walimu wa shule za umma na kukuta kiwanja chao kikiwa kimeuzwa na hata kuwekwa uzio.
Shule hio ina karibu watoto 1,000 walio kati ya umri wa miaka mitatu na 14 na inasimamiwa na Halmashauri ya Jiji.
Wanafunzi kadhaa wamejeruhiwa katika purukushani hizo wakati polisi walipoingilia kati na kujaribu kuwatawanya wanafunzi hao waliokuwa wanazua vurugu. Baadhi yao walipelekewa hospitalini baada ya kupata majeraha madogomadogo.
Baadhi ya wanafunzi hao walikabiliana na polisi wakiwa wamebeba fimbo ambapo polisi mmoja alijeruhiwa baada ya kupigwa kwa mawe.
BBC