Thursday, January 15, 2015

NYALANDU AKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA SAUDI ARABIA KUWEKEZA SEKTA YA UTALII NCHINI


NYALANDU AKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA SAUDI ARABIA KUWEKEZA SEKTA YA UTALII NCHINI
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kushoto) akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia Dk. Abdulrahman Al-Zamil (wa tatu kushoto) jijini Riyadh, Saudi Arabia. Wengine katika picha kutoka kulia ni Mshauri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Saudia Mohammad Sulayem; Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Prof. Abdillah Omari.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia Dk. Abdulrahman Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mhe. James Lembeli (kushoto) akikaribishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil jijini  Riyadh, Saudi Arabia.
 Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe. Peter Msigwa (kushoto) akikaribishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (wa tano kushoto) ukiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al- Zamil (wa sita kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya pande mbili jijini Riyadh, Saudi Arabia. Wengine pichani kutoka kushoto ni pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori Herman Keraryo; Mkurugenzi Mkuu TANAPA Allan Kijazi; Mhe James Lembeli; Mhe Peter Msigwa; Katibu Mkuu Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru pamoja na maafisa kutoka Chemba ya Biashara ya  Saudia.                                                                                          

 Na Pascal Shelutete, TANAPA

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Saudi Arabia kuwekeza katika sekta ya utalii nchini ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji. Nyalandu alitoa wito huo kufuatia mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Saudi Arabia Dk. Abdulrahman Al-Zamil yaliyofanyika Riyadh, Saudi Arabia jana.

Waziri Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Saudia alibainisha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanavutia na kutaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli na loji za kisasa zitakazoweza kuvutia watalii wengi zaidi katika maeneo ya mijini pamoja na ndani ya maeneo ya uhifadhi.

Alisema kuwa utalii wa Tanzania unakua kwa kasi nzuri kutokana jitihada zinazofanywa na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kutangaza vivutio vya utalii na kuwa juhudi hizo lazima ziende sambamba na upatikanaji wa huduma bora za malazi. "Upatikanaji wa huduma nzuri za malazi ya bei nafuu utasaidia kuvutia watalii wengi zaidi nchini na kwa maana hiyo tunawakaribisha kuja kuzitumia fursa zilizopo ili kuweza kukuza uchumi wa nchi yetu", alisema Nyalandu.

Waziri Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Saudia, alisema kuwa Tanzania ni ya pili ulimwenguni baada ya Brazil kwa kuwa na vivutio vizuri vya asili vya utalii na kuwa rasilimali hizi zinapaswa sasa kutumiwa vema ili kuinua uchumi na njia pekee ni pamoja na kuvutia wawekezaji na mitaji kutoka Saudia ili kufikia azma hiyo.
Kwa upande wake Dk. Al-Zamil aliahidi kuwashirikisha wafanyabiashara wenzake kutikia wito huo na kwa kuanzia timu ya wafanyabiashara pamoja na mawakala wa utalii watafika nchini katika siku chache zijazo ili kuona namna gani wataweza kuzitumia fursa zilizopo kikamilifu. Aidha, katika eneo la utalii Al- Zamil alisema kuwa Chemba yake itafanya kila liwezekanalo kubadilisha mtazamo wa Wasaudia wanaotembelea kwa wingi maeneo mbalimbali ya utalii duniani ili waweze kuitembelea Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru alisema kuwa serikali itaandaa Kongamano Maalum la Uwekezaji nchini Saudi Arabia ili kuweza kutangaza fursa mbalimbali zzilizopo nchini ambazo zikitumika vema zinaweza kuinua uchumi wa taifa.

Hivi sasa Tanzania inategemea idadi kubwa ya watalii kutoka Mataifa ya Ulaya na Amerika na kwamba japokuwa idadi ya watalii kutoka nchi za kiarabu haizidi 15,000 kwa mwaka, bado jitihada za utangazaji na uwekezaji zikifanywa vizuri idadi ya watalii kutoka mataifa ya kiarabu itaweza kuongezeka nchini.

Ujumbe wa Tanzania unajumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru; Balozi wa Tanzania Saudi Arabia Prof. Abdillah Omari; Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mhe. James Lembeli, Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe. Mchingaji Peter Msigwa; Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Allan Kijazi pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Herman Keraryo.