JUMATATU ya wiki hii, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), lilisaini mkataba wa miaka 18 na klabu kubwa na tajiri duniani, Real Madrid kujenga kituo cha michezo nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau, shirika hilo limetenga zaidi ya ekari 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kitakachoitwa NSSF- Real Madrid Sports Academy.
Shirika hilo limekwenda mbali zaidi kwa kujenga kijiji cha michezo katika eneo hilo kitakachoitwa NSSF Sports City ambapo kitakuwa na huduma mbalimbali za kijamii kama maduka, benki na vitu vyote muhimu.
Aidha, Dk Dau alisema kituo hicho kitaanza kujengwa Mei mwaka huu na wakati ujenzi ukiendelea, kituo kitaanza kufanya kazi kwenye majengo ya kukodi.
Dk Dau aliwaambia waandishi wa habari kwamba shirika lake limeamua kuwekeza rasmi kwenye michezo na kituo hicho ni moja ya maandalizi ya safari ya Tanzania kushiriki michuano ya Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa Dk Dau, ikiwezekana fainali za Qatar mwaka 2022, Tanzania ishiriki, kutoka kwa watoto watakaopikwa kwenye kituo hicho chini ya makocha mahiri wa Real Madrid.
Naipongeza NSSF kwa uamuzi wa kuwekeza kwenye michezo na sasa wadau wengine wenye kutaka mafanikio katika michezo wawaunge mkono kwa kuwa wadhamini wenza katika kujenga kituo hicho.
Lengo la NSSF si kuwekeza kwenye soka pekee, bali michezo yote na ndio maana kwa mujibu wa michoro ya kituo hicho, kutakuwa na viwanja vitano ukiwemo uwanja wa gofu.
NSSF wamesema wanalifanya hilo kama biashara na si hisani, lengo lao kuuza wachezaji nje ya nchi, jambo ambalo naamini kila mpenda maendeleo ya nchi analitamani.
Real Madrid ni moja ya timu zinazovuna fedha nyingi kutokana na umaarufu na mipango yake katika soka. Kwa mwaka, inavuna Dola za Marekani milioni 675, hivyo kwa jambo hili lililofanywa na NSSF, upo uwezekano mkubwa wa Tanzania kufanya vizuri na pia kufahamika kimataifa.
Tumekuwa wasindikizaji mara zote kwenye michezo yote, pengine ujio wa kijiji hicho cha NSSF utaleta mabadiliko na kutoa mwanga kwa vipaji vipya.
Wachezaji kadhaa wanakosa nafasi za kucheza nje pengine hili linatokana na kutokuwa na uzoefu, hivyo kwa kuwa na kijiji hicho cha michezo, wachezaji wetu watafunzwa mambo kadhaa ya kufanya na kuzivutia timu kubwa nje zitakazofanya biashara na baadaye kuitangaza Tanzania.
Kituo hicho kinatarajiwa kuchukua watoto kuanzia umri wa miaka chini ya 13, 18, 20, timu B na timu ya wakubwa. Ni matumaini yangu pia kwa upande wa wachezaji, huu ni wakati wao wa kuonesha vipaji na kupata maslahi kwenye michezo badala ya kulalama kila kukicha kwamba michezo hailipi.
Naamini ujenzi wa kituo hicho ni mwanzo, wapo wengine watakaojitolea kujenga vituo ama vijiji vya michezo kama hivyo ili viwe vingi nchini kuondoa ukosefu wa ajira nchini na hata wimbi la utumiaji wa dawa za kulevya.