Friday, January 16, 2015

Mkopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakomboa Kikundi cha Iringa Promise Keepers


Mkopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakomboa Kikundi cha Iringa Promise Keepers
Afisa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Chamwino Bw. Denis Vagela (kushoto) akizungumza na Vijana wa kikundi cha Wajasiriamali wa Wilaya ya Chamwino wanaojishughulisha na utengenezaji wa Sabuni za maji, Batiki na ufundi walipotembelewa kwa ajili ya kuangalia mradi wao leo Mkoani Dodoma. Katikati ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa, na aliyekaa ni Afisa Vijana Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga.
Wakwanza mbele ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa akiangalia mashine ya kukamua alizeti iliyotengenezwa na Vijana wa kikundi cha Chachu ya Maendeleo Dodoma wakati wa kutembelea miradi ya vijana wa Mkoa wa Dodoma. Kulia ni kijana wa kikundi hicho Bw. Ayoub Athumani.
Kijana Samwel Nagija kutoka kikundi cha vijana cha Chachu ya Maendeleo Dodoma kinachojishughulisha na utengenezaji wa mashine za kusaga na kukoboa, mashine za kutengeneza matofali, mashine za kukamua alizeti, na ujenzi wa vitanda na madawati ya chuma akiendelea na ujenzi wa mashine ya kusaga leo Mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Iringa Promise Keepers Bw. Rashid Magule (kushoto) kinachojishughulisha na ufundi Selemala akielezea namna kikundi chake kilivyofaidika na mkopo unaotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Wanaomsikiliza kutoka kulia ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa, anayefuata ni Afisa Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga na wapili kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw.Laurean Masele. (Picha na Genofeva Matemu – Maelezo, Dodoma)

Na Genofeva Matemu

Vijana kutoka kikundi cha Iringa Promise Keepers chenye wanachama 6 wanaojishughulisha na ufundi Selemala wameishukuru Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwapatia mkopo wa shilingi laki tatu mwaka 2007 ambao umeinua na kusababisha mradi wa kikundi kupanuka na kuwa mkubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kikundi hicho Bw. Rashid Magule walipotembelewa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na maafisa kutoka ofisi ya Mkoa wa Dodoma kukagua miradi ya vijana leo Mkoani Dodoma.

"Kikundi cha Iringa Promise Keepers kinaishukuru Serikali kwa kutufaidisha na mkopo wa shilingi laki tatu kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana tuliopatiwa mwaka 2007 ambao ulikua kama mtaji katika kikundi chetu hivyo kupanuka na kuwa na mtaji wa shilingi milioni nne unaotuwezesha wanakikundi kupata kipato cha kuweza kuendesha maisha yetu" alisema Bw.   Magule.

Hata hivyo Bw. Magule ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuendelea kukipatia mkopo kikundi chake kwani bado wanakikundi wanahitaji kujiendeleza zaidi na kuwaendelezo vijana wenzao wanaohitaji utaalamu kutoka kwao hivyo kuomba kupatiwa mkopo wa shilingi milioni mbili kwa ajili ya maendeleo ya kikundi hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya kilichopo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Laurean Masele amewapongeza wanakikundi kwa jitihada kubwa walizozifanya na kuweza kutumia mpoko mdogo waliopata kusimamia na kuendeleza mradi wao kwa kushirikiana.

Bw. Masele amewashauri wanakikundi kufanya kazi kwa ushirikiano huo huo huku wakisimamia malengo waliyokusudia kwa kutumia ujuzi walionao kwani vijana wakiwezeshwa wanaweza.

Naye Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Dodoma Bw. Tumsifu Mwasamale amewapongeza wanakikundi wa Iringa Promise Keepers kwa maendeleo waliyonayo na kuwataka kutafuta eneo lao binafsi kwa ajili ya shughuli zao kwani mradi wao unahitaji nafasi kubwa na ya wazi itakayosaidia kuonyesha bidhaa wanazozalisha katika jamii.