Saturday, January 10, 2015

MHADHIRI WA CHUO CHA CBE KORTINI AKIDAIWA KUTISHIA KUUA KWA RISASI



MHADHIRI WA CHUO CHA CBE KORTINI AKIDAIWA KUTISHIA KUUA KWA RISASI

 MHADHIRI Msaidizi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Andrew Kimbombo (52) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na mashitaka ya kutishia kuua wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kimbombo ambaye pia ni Mjumbe wa Serikali za Mitaa Kata ya Kiwalani, Dar es Salaam, alisomewa mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda alidai kwamba Desemba 21 mwaka jana, maeneo ya Kiwalani Migombani, Kimbombo alitishia kumuua kwa kumpiga risasi, Bakari Mussa huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande. Kesi itatajwa Januari 23 mwaka huu. Wakati huo huo, wafuasi 10 wa vyama vya Chadema, CCM na CUF waliodaiwa kufanya vurugu wakati wa uapishaji wa wenyeviti wa Serikali Mitaa kata ya Ubungo, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kujeruhi na kuwazuia askari kufanya kazi.

Washitakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mbele ya mahakimu mawili tofauti. Awali, Sunday Urio (20), Kizito Damian (35), Joseph Sanky (30), Chrisant Luhilila (24), Karim Ally (40, Wilfred Ngowi (30) na Kinyaiya Siriri (35) walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka.

Wakili wa Serikali Tumaini Kweka akisaidiwa na Janeth Kitali alidai Januari 6 mwaka huu katika eneo la Ubungo Riverside, washitakiwa waliwarushia mawe askari wa jeshi la polisi kwa lengo la kuwazuia wasitekeleze majukumu yako ya kutuliza amani.

Katika hatua nyingine, Abdul Hamis (67), Mwanahamisi Salum (42) Sandro Carlos, Damian, Sanky, Urio na Ally walisomewa mashitaka ya kujeruhi mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda.
Wakili Kitali alidai, siku hiyo hiyo katika Hoteli ya Landmark Riverside, washitakiwa walimjeruhi Juma Salum kwa kutumia mawe, jambo lililomsababishia maumivu na kuvunjika mkono wa kushoto.

Washtakiwa walikana mashitaka na Hamis, Mwanahamisi na Carlos walipata dhamana baada ya kutimiza masharti na washitakiwa wengine walirudishwa rumande hadi barua za wadhamini wao zitakapokaguliwa.

Upelelezi wa kesi hizo umekamilika na zimeahirishwa hadi Januari 21 mwaka huu, washitakiwa watakaposomewa maelezo ya awali. Pia, wakala wa CCM, Anna Shitundi (32) amepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo akikabiliwa na mashitaka ya kufanya fujo na kuharibu kasha la kupigia kura.

Wakili wa Serikali Anunciatha Leopold alidai Desemba 21 mwaka jana, maeneo ya Vingunguti Fani 'B', mshitakiwa alipiga teke kasha la kupigia kura na kulipasua mfuniko kitu ambacho kilisababisha usumbufu kwa msimamizi wa uchaguzi huo.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

 Alitakiwa kuwa na wadhamini wawili, mmoja kutoka taasisi inayotambulika, watakaosaini kulipa Sh milioni 2.
Ilidaiwa kwamba mshitakiwa alifanya hivyo wakati wa kuhesabu kura baada ya msimamizi wa CUF kuongeza kura mbili ilihali wakiwa wameshinda katika uchaguzi huo na kusababisha vurugu pamoja na kuharibu kasha la kupigia kura.

Kesi itatajwa Januari 19 mwaka huu. CCM, CUF washutumiana Kufuatia vurugu za uchaguzi wa serikali za mitaa hadi kuapishwa kwa wenyeviti wake na kusababisha baadhi ya watu kupigwa na sehemu nyingine polisi kutuliza ghasia navyo vyama vya CCM na CUF vimeshutumiana kila kimoja kuwa chanzo cha vurugu hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari jana, viongozi wa vyama hivyo wameeleza sababu mbalimbali za matukio hayo kusababishwa na upande mwingine.
Kwa upande wa CCM, kimelaani vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na wakati wa uapishwaji wa wenyeviti wa mitaa hiyo, huku kikishutumu vyama vya upinzani kuratibu vurugu hizo.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo uliofanyika Desemba 14, mwaka jana na zile zilizojitokeza wakati wa uapishwaji wa wenyeviti wa serikali za mitaa wa Kinondoni pamoja na Ilala ziliratibiwa na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema, viongozi wa vyama vya upinzani ndio wamekuwa wahusika wa vurugu hizo, huku akidai huo ni mwelekeo wa kufa kwa vyama hivyo.

Alisema katika vurugu zilizojitokeza licha ya kuvuruga taratibu zilizowekwa ikiwemo za kuwaapisha wenyeviti wa baadhi ya maeneo, pia zimesababisha uharibifu wa mali na kujeruhiwa kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali.

Akifafanua kujeruhiwa kwa viongozi wao, Nape alisema, Christopher Mgeta wa mtaa wa Ibungilo na Padscala Charles wa Kitangiri 'A' mkoani Mwanza walivamiwa na kupigwa wakati wa kuapishwa.

Hata hivyo alisema chama hicho hakitaweza kuendelea kuvumilia kuona vurugu hizo zinafanyika tena, huku akivitaka vyama hivyo kukoma na kuacha tabia hiyo ya kufanya vurugu kwa kuwa njia pekee ni kukaa na kujipanga badala ya kufanya vurugu.

Nacho Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Magdalena Sakaya alidai kuwa vurugu hizo zinatokana na watendaji kupewa maagizo na serikali inayoongozwa na CCM.

Alitoa mfano wa maeneo kadhaa yaliyosababisha vurugu kuwa ni pamoja na mtaa wa Mwinyimkuu katika manispaa ya Kinondoni ambapo baada ya uchaguzi kufanyika siku iliyofuata msimamizi wa uchaguzi alimtangaza mgombea wa CUF, Hassan Mwinchumu kuwa mshindi, lakini jambo la kushangaza msimamizi wa uchaguzi katika manispaa hiyo aliitisha uchaguzi mwingine ambapo CUF waliugomea.

Alisema baada ya kugomea msimamizi wa uchaguzi akamtangaza mgombea wa CCM, Funua Ally Funua kuwa mshindi na wananchi kumkataa ndipo wakazuia kuapishwa kwake na kusababisha vurugu.

Alisema katika mtaa wa Ukwamani katika Manispaa ya Kinondoni, CUF ilishinda na mgombea wake kutangazwa mshindi lakini fomu za matokeo hazikusainiwa hadi leo, lakini wakati wa kuapishwa mgombea wa CCM ndiye alipewa barua jambo ambalo wananchi walizuia na hakuna mgombea aliyeapishwa.

Na katika mtaa wa Msisiri Mwananyamala, mgombea wa CUF alitangazwa mshindi lakini kesho yake ikabandikwa matokeo yanayoonesha CCM walishinda na kupewa barua ya kuapishwa pia wananchi walizuia kwa kuwa hawakumchagua.

Alisema katika mtaa wa Kiwalani, kata ya Migombani na Kigogo Fresh, matokeo hayakutangazwa kwa sababu mbalimbali lakini wagombea wa CCM walipewa barua za kuapishwa.
Sakaya alisema mitaa mingine iliyokumbwa na utata ni Malapa, Kinyerezi, Migombani na Bunda mkoani Mara na kwingineko na malalamiko yanaendelea kupokelewa nchi nzima.

Polisi yatoa onyo Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, limetoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kufanya fujo na vitendo vya vurugu ikiwemo kuwapiga baadhi ya watendaji wanaosimamia utaratibu wa kuapisha pamoja na kuwapiga viongozi wateule waliochaguliwa kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema Jeshi la Polisi linawataka wakurugenzi na maofisa watendaji wenye dhamana ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti waliochaguliwa, kufuatilia kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua migogoro hiyo mapema ili kuepusha migongano inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema jeshi la Polisi halitamvumilia mtu ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu ama fujo kwa kisingizio cha ushabiki.