Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na viongozi katika kuchangia nguvu za kukabiliana na matatizo mbali mbali yanayowakabili wananchi katika maeneo yao lakini bado jukumu hilo litaendelea kubakia mikononi mwa wananchi wenyewe.
Alisema Viongozi na hata Serikali Kuu huhamasika na kushawishika zaidi kusaidia hata uwezeshaji na hata vifaa kwenye miradi ya Jamii baada ya kuona nguvu za Wananchi zimeanza au kuiendelezwa katika kujikomboa na umaskini au kujitafutia maendeleo yao.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akikabidhi mabomba 250 ya kusambazia huduma za maji safi na salama yaliyogharimu jumla ya shilingi Milioni 17,000,000/- kwa ajili ya Wananchi wa Kijiji cha Kilombero hapo katika kituo cha Kilimo Kilombero Wilaya ya Kaskazini " B " Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Kilombero kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kujiondoshea matatizo yanayowakabili ikiwemo kushiriki katika kazi za usambazaji wa huduma za maji safi.
Aliwaeleza wananchi hao wa Kijiji cha Kilombero kwamba jitihada zitaendelea kuchukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo za kusambazwa huduma za maji safi na salama katika mitaa ya kijiji hicho mara baada ya Bomba za maji hayo kufikishwa katika eneo la Skuli ya Kilombero kutoka kwenye kisima hicho.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Kilombero Msimamizi wa Kamati ya mradi wa Maji ya Kijiji hicho Bwana Moh'd Haji Faki alimuhakikishia mbunge huyo wa Jimbo la Kitope kwamba Wananchi wa Kijiji hicho wako tayari muda wowote kushiriki katika kazi za maendeleo wakati watapotakiwa kufanya hivyo.
Zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi zimetumika katika ujenzi wa Kisima cha Maji ya Kilombero kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu wa miaka mingi wa huduma za upatikanaji wa maji safi na salama wananchi wa Kijiji hicho.
Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mabomba ya kusambazia maji safi Diwani ya Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla Mussa kwa ya Kijiji cha kilombero Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kati kati yao ni Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleiman Iddi.
Mabomba ya kusambazia maji safi katika Kijiji cha Kilombero yenye gharama ya shilingi Milioni 17,000,000/- yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitopo Balozi Seif Ali Iddi.
Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishiriki katika kazi ya uchimbaji mtaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba kwa ajili ya huduma za kusambazaji wa maji safi katika Kijiji cha Kilombero. Picha na Hassan Issa wa – OPMR – ZNZ.