Thursday, December 11, 2014

WALAJI WA MBOGA DAR KIFO KINAWANYEMELEA




WALAJI WA MBOGA DAR KIFO KINAWANYEMELEA

Wakazi WA jiji la Dar es Salaam wako katika hatari ya kupatwa na magonjwa makubwa kama saratani, utasa, kupoteza uwezo wa kuona, kuharibu ubongo, maini na figo, kutokana na matumizi ya mboga za majani zinazolimwa katika mabonde ya jiji hilo, NIPASHE imebani


Matumizi ya mboga hizo ni makubwa jijini humo, yakitokana na umuhimu wake kwa afya za watu na hali duni ya maisha inayozifanya familia nyingi kumudu gharama zake ikilinganishwa na vitoweo vingine.

Sehemu kubwa ya mboga hizo inatokana na kilimo kinachofanyika kwenye bonde la Mto Msimbazi na maeneo ya Kigogo-Sambusa, Ubungo--Gereji, Mchicha – Vingunguti na Tandale.

Tayari matokeo ya tafiti kadhaa yamedhihirisha maji yanayotumika kwa umwagiliaji wa mboga za majani jijini humo kuwa na kemikali zenye sumu ama taka zinazotoka viwandani na kwenye makazi ya watu.

Pia, baadhi ya wakazi wanaoishi pembezoni mwa bonde la Msimbazi na maeneo mengine yanayolimwa mboga hizo, wamebainika kutupa taka kama betri zilizoisha muda wa matumizi, masalia ya simu za mkononi, vipuri vya magari na majokofu mabovu.

Taka hizo zenye sumu kali, zinatupwa kwenye mifereji ya maji yanayotumika kwa umwagiliaji wa mboga hivyo kuzidi kuhatarisha afya za walaji.

TAFITI  MBALIMBALI
Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), kilifanya utafiti katika bonde la Mto Msimbazi wilayani Ilala mwaka 2010, kwa kupima maji, udongo na maji, kwa vigezo vya Shirika la Afya Duniani (Who) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akizungumzia utafiti huo, Mhadhiri wa Uhandisi wa Mazingira kutoka Aru, Dk. William Mwegoha, anasema waligundua mabwawa ya majitaka yanayotoka Mabibo, dampo la Vingunguti, viwandani na gereji mbalimbali yanamwaga maji kwenye mto huo.

"Baada ya kupima maji hayo, tulikuta yana madini ya shaba, risasi, kromiamu na ladimiamu ambazo ni sumu kwa mlaji," anasema.

Dk. Mwegoha anasema mboga zilizomwagiwa maji hayo zilibainika kuwa na sumu iliyotokana na madini ya risasi, shaba na kromiamu ambazo zote zina madhara kwa binadamu.

Alisema utafiti huo ulihusisha wakulima 35 wa maeneo ya Jangwani, Kigogo, Vingunguti na Tabata Shule, ambao wanatumia maji ya mto huo kumwagilia mboga za majani.

Dk. Mwegoha alisema katika utafiti huo walibaini kuwa  mboga hizo zinauzwa zaidi kwenye masoko ya Ilala, Kariakoo, Buguruni, Vetenari, Tazara, Mwananyamala, Mnyamani, Kigogo, Kisutu, Vingunguti, Tabata, Mikoroshini na maeneo ya jirani na wakulima hao.

Pia anasema kwa mujibu wa utafiti huo, mboga hizo zinauzwa pia kwenye masoko ya maeneo mengine ya jijini humo.

Alisema licha ya Vingunguti kukuta bango kubwa likitoa hadhari kwamba maji ya mto huo siyo salama kwa matumizi ya binadamu, wanyama na kumwagilia mazao, bado wakulima walibainika kuendelea kuyatumia.

Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 71 ya wakulima wa mboga za majani wanatumia maji hayo na asilimia 63 hawajui kama yana madhara na hayafai kumwagilia mazao, huku asilimia mbili wakisema wanafahamu kuwa yana sumu.

Mhadhiri huyo anasema wakulima hao wanapata kipato cha kuendesha maisha yao ambapo kwa wastani kwa mwezi mmoja, mkulima anapata pato la kati ya Sh 89,000 hadi 300,000 kutokana na biashara hiyo.

Licha ya kugundulika kuwa na sumu inayotoka viwandani, maji mengine yanayotumika katika umwagiliaji wa mboga hizo yamebainika kuchanganyika na majitaka yakiwamo yanayotoka kwenye vyoo. Umwagiliaji huo unafanyika kuanzia kupanda mbegu hadi uvunaji wa mboga.

Peter Mwakikao ni mmoja wa wananchi wanaoishi Ubungo- Gereji, anasema kwa muda mrefu sasa mifereji ya maji machafu imekuwa ikitiririsha maji kutoka viwandani kwenda kwenye mashamba ya mboga za majani na makazi ya watu.

Licha ya matumizi ya maji hayo, inaelezwa kuwa wakulima wa mboga wanatumia dawa za kukuzia na kuua wadudu isivyostahili, hivyo kuzidi kuhatarisha afya za watumiaji wake.
Sehemu ya matumizi ya dawa hizo inaelezwa kulenga kujinufaisha kujipatia kipato kwa kutumia madawa yanayokuza mboga kwa muda mfupi.

 WAKULIMA
Hata hivyo wakulima kadha
iwamo wasiotaka majina yao kutajwa gazetini, wanataja ukosefu wa maji salama kwa umwagiliaji kuwa chanzo cha matumizi ya maji yasiyofaa kwa mimea na matumizi ya binadamu.

"Hatuna namna nyingine zaidi ya kutumia maji hayo… hakuna maji salama kwa umwagiliaji wa mboga hizi, na kwa vile maisha yetu yanategemea rasilimali hii hatuwezi kuacha," anasema mmoja wa wakulima hao eneo la Keko Mwanga.

Anasema mbadala wa maji hayo ni wakati mvua zinaponyesha na si vinginevyo.

Naye Munga Mkude mkulima katika bonde la Keko Mwanga, anasema ipo haja kwa serikali kuingilia kati na kubuni miradi ya ujenzi wa visima virefu vitakavyo wawezesha kushiriki kilimo cha umwagiliaji usiokuwa na madhara kwa mboga na afya za watu.

Kwa upande wake, mkulima Asumile Mwakasala, anasema pamoja na kutumiwa na wananchi wa kawaida, mboga wanazozilima zimekosa soko kwenye maduka makubwa maarufu kama Super Markets.

Kutokana na ukosefu wa soko hilo, wakulima hao wamewekeza zaidi kwa wafanyabiashara wanaonunua na kuziuza kwenye masoko na makazi ya watu jijini humo.
Pamoja na hatari hiyo, wapo wakulima akiwamo Lusako William wa Tabata Gereji waliochimba visima vipufi kwa ajili ya kupata maji ya umwagiliaji mboga hizo.
Hata hivyo, NIPASHE ilipotembelea visima hivyo ilibaini kuwa ni vifupi na maji yaliyomo ni yale yanayotoka viwandani yakiwa na kemikali zenye sumu.

KAULI YA TFDA
Afisa uchanganuzi wa madhara yanayotokana na  chakula katika Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Kaiza Kilango, anasema serikali inaendelea kukusanya mboga zinazouzwa kwenye masoko kadhaa jijini humo ili kuzipima.

Anasema hatua hiyo inalenga kubaini ikiwa kuna mboga za majani zilizoathirika kwa kemikali ama kuwa na vimelea vya magonjwa, hivyo kuwasiliana na maofisa kilimo wa halmashauri husika.

"Huwa tunapita masokoni na tunanunua bidhaa kama wateja wa kawaida, tukishazipima na kubaini zenye madhara tunawataarifu wakurugenzi na maofisa kilimo ili wachukue hatua," anasema Kilango.

Anasema TFDA hawana uwezo wa kuwazuia wakulima kumwagilia mboga kwa kutumia maji yenye kemikali zenye sumu ama maji machafu kwa kuwa wajibu huo upo kwa mamlaka za halmashauri za manispaa. Mbali na halmashauri za manispaa, Kilango, anasema taarifa za ukaguzi huo zinawasilishwa kwa Baraza la Taifa la Hifadhi la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) ili kuchukua hatua dhidi ya kiwanda husika.

"Sisi tunaendelea na tutaendelea kuelimisha watu hususani wakulima wenyewe wasitumie maji yanayotoka viwandani kwa kuwa mara nyingi si salama kwa afya ya binadamu." anasema.

CHANZO: NIPASHE