Saturday, December 13, 2014

TAMISEMI YAWEKA BAYANA utaratibu utakaotumika hapo kesho wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa



TAMISEMI YAWEKA BAYANA utaratibu utakaotumika hapo kesho wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini akiwaeleza waandishi wa Habari kuhusu utaratibu utakaotumika hapo kesho wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa mbili asubuhi (2:00) hadi saa kumi alasiri (10:00) ambapo wananchi wote watakaokuwepo vituoni hadi kufikia muda huo wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemalizika.Kushoto ni Mratibu wa uchaguzi huo bw.Denis Bandisa

FRANK MVUNGI-MAELEZO
Serikali imewataka wananchi wote waliojiandikisha  kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa  kushiriki kwa wingi ili waweze kuwachagua viongozi wao katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam .
Akifafanua Sagini amesema wapiga kura wazingatie kuwa kila mpiga kura anatakiwa kupiga kura moja tu na apige kwenye kitongoji au mtaa anaoishi  na si vinginevyo.
Pia Sagini alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, Asasi zisizo za Kiserikali kuwahamasisha wapiga kura kujitokeza kwa wingi hapo kesho kuchagua viongozi wao.
Akiwatahadharisha wananchi kuhusu kupiga kura Zaidi ya mara moja au kutaka kupiga kura wakati  si mkazi wa eneo hilo  Sagini alisema  hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaojaribu kukiuka sheria, Kanuni na taratibu za uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo sagini alibainisha kuwa utaratibu utakaotumika ni kupiga kura,kuhesabu na kutangaza matokeo ambapo taratibu zote zimefafanuliwa katika Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2014 na katika mwongozo wa uchaguzi huo.
Wapiga kura wote wametakiwa kufika katika maeneo ya kupigia kura wakiwa na kitambulisho cha mpiga kura cha Uchaguzi Mkuu, Kitambulisho cha kazi,Hati ya kusafiria,Kadi ya benki,Kadi ya Bima ya Afya,Kitambulisho cha shule au chuo,Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha uraia kwa ajili ya kuwatambulisha.

Uchaguzi wa Serikali za mitaa katika ngazi za vijiji,Mitaa na vitongoji utafanyika siku ya jumapili ya tarehe 14 Desemba,2014 ambapo katika uchaguzi huo watachaguliwa wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa Halmashauri za Vijiji,Wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za mitaa na wajumbe wa kamati za Mitaa na wenyeviti wa vitongoji.