Na Fredy Mgunda,Iringa
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Frank Kibiki, ametangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo la Iringa mjini, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa Habari leo ofisini kwake, Kibiki amesema ni wakati wa vijana kushika hatamu kwa kuwania nafasi mbali mbali, ndani ya CCM na hatimaye kwenye umma wa watanzania.
Kibiki ambaye ni Katibu mwandamizi wa Umoja wa Vijana, katika wilaya mbali mbali nchini amesema ameamua kuomba kupitishwa nafasi hiyo na CCM ili aweze kusaidiana na wananchi wa manipaa ya Iringa katika kuwaletea maendeleo.
Mjumbe huyo wa Mkutano mkuu wa ccm Taifa, amedai kuwa zipo changamoto nyingi zinazowakabili vijana na wananchi kwa ujumla na kwamba, njia pekee ya kuzitatua ni kuwa na uwakilishi toka miongoni mwao kwenye vyombo vya maamuzi.
Kitaaluma, Kibiki ni mwandishi wa habari mwandamizi kupitia magazeti ya Uhuru na Mzalendo, mkoani Iringa.