Na matukiodaimaBlog MKURUGENZI wa kampuni ya ujenzi wa barabara nchini ya GNSM Contractors Co. Ltd ya mkoani Iringa ametoa msaada wa chakula chenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 1.5 kwa kituo cha kulea watoto yatima cha Tosamaganga katika wilaya ya Iringa kwa ajili ya sikukuu ya Krismas na mwaka mpya . Huku akiwapongeza wahudumu wa kituo hicho kwa kuendelea kuifanya kazi hiyo ya kulea watoto zaidi ya 70 waliopo kituoni hapo kwa moyo wa kujitoa zaidi. Mkurugenzi huyo Geofrey Mungai ambae aliongozana na mkewe Bi Sarafina Mungai alikabidhi msaada huo jana ikiwa ni sehemu ya mwensdelezo wa kampuni hiyo na familia yake kuzungukia vituo mbali mbali vya yatima kwa kuwasaidia watoto hao. Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo Bw Mungai alisema kuwa imekuwa ni kawaida ya kampuni yake kuwakumbuka watoto hao yatima wa kituo hicho na vituo ikiwa ni moja ya kuwakumbuka watoto hao ambao wanaishi kwa kutegemea misaada ya wasamaria wema. Alisema kuwa jamii inapaswa kubadilika kwa kuelekeza michango yao kwa watoto yatima ambao wanaishi kwa misaada ya wahisani wa ndani na nje baada kupoteza wazazi wao . Kwani alisema kuendelea kuwasaidia watoto hao ni kuwasogezea faraja ya pekee ambayo watoto hao wanahitaji kutoka kwa jamii inayowazunguka badala ya kuwasusa ama kuwaachia watu wachache kulea yatima hao. Aidha alisema kuwa yeye kama mmoja kati ya makandarasi mkoa wa Iringa anaendelea kufanya mazungumzo na wenzake ili kuweka mpango wa kuendelea kutembelea vituo vya yatima kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia misaada mbali mbali. Huku akiishauri serikali kuangalia uwezekano kupitia ofisi za maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuweka utaratibu wa kuwakumbuka watoto waliopo katika vituo vya yatima kwa kuwapa mahitaji yao ya kila siku . Bw Mungai alipongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na uongozi wa kituo hicho cha Tosamaganga ambacho sehemu kubwa watoto wanaolelewa hapo ni wale wanaotupwa ama wazazi wao kufariki baada ya kuwazaa. Alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa watoto hao yatima kuendelea kusaidia iwapo watanzania na wadau mbali mbali wakiwemo makandarasi wenzake kuwekeza kwa watoto hao Kwa upande wake Bi Sarafina Mungai akizungumza na wahudumu hao alisema kuwa kazi wanayoifanya ni kazi kubwa ambayo serikali na wananchi hawanabudi kuitambua na kuwaunga mkono zaidi. |