Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewasili nchini Uturuki kwa ziara ya siku tatu ya kiserikali.
Ziara hiyo inafuatia mwaliko rasmi wa serikali ya Uturuki kupitia kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Ahmet Davutoglu.
Kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa mjini Istanbul, Maalim Seif alipokelewa na Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Mhe. Mevlut Cavusoglu.
Mbali ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake ambaye ni Waziri Mkuu wa Uturuki, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa jumuiya ya watembezaji watalii ya nchi hiyo.
Aidha Maalim Seif ambaye ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Bw. Ali Saleh Mwinyikai, anatarajiwa kuhudhuria kwenye maadhimisho ya sherehe kubwa za kimila nchini humo ambazo pia zitahudhuriwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Recep Tayyip Erdogan.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na wageni kadhaa mashuhuri kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais
Zanzibar.