Friday, December 19, 2014

KUJIAJIRI NI FURSA PEKEE YA MAENDELEO


KUJIAJIRI NI FURSA PEKEE YA MAENDELEO
Beatrice Lyimo -Maelezo

Serikali imewashauri wahitimu kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini kwani inatambua ukosefu wa ajira nchini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar ea Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya  Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Willium Lukuvi alipokuwa akifungua kongamano la mafunzo kwa wajasiliamali wadogo wadogo.

Amesema  kuwa vijana wanatakiwa kuweka mkazo katika suala la ujasiriamali na kujihusisha na mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali ili kuwa na fursa mbalimbali kiuchumi.

"Mtazamo chanya, kujitambua, kuwa wabunifu na kusema inawezekana vinachangia kuzidisha maendeleo binafsi hivyo kila kijana afikirie kuwa anaweza"  aliongeza  Waziri Lukuvi.
Mbali na hayo Waziri Lukuvi alisema kuwa vijana hawana mitaji ya kujiendeleza  lakini taasisi za kifedha zinauwezo wa kuwakopesha iwapo watakua na vitambulisho vya Taifa na anwani za makazi hivyo kupelekea vijana kujiajiri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wajiri nchini Bw. Almasi Maige amewaasa wahitimu kuwa na mawazo chanya na kufikiria zaidi kuhusu kujiajiri na si kusubiri kuajiriwa.
"Hakuna ujasiriamali rahisi, inatakiwa kujitoa haswa kwa watu ama vijana wenye nguvu kama ninyi" aliongeza Maige.

Hivyo kuwashauri vijana kuwa wabunifu na kuanzisha shughuli zitakazosaidia kuongeza kipato na si kutegemea kukopi kutoka sehemu nyingine.

Kongamano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Gilgal nchini yenye  kauli mbiu isemayo "wajasiriamali wadogo fursa zilizowazi" lenye lengo la kubadili fikra kwa vijana walio vyuoni kutumia fursa zilizopo.