Monday, December 01, 2014

Kampuni ya AFRICAN BARRICK GOLD yabadili jina,sasa kuitwa “Acacia”




Kampuni ya AFRICAN BARRICK GOLD yabadili jina,sasa kuitwa "Acacia"
Kampuni ya African Barick Gold (ABG) inayo furaha kutangaza kuwa imebadili jina lake na sasa na itatambulika kama Acacia Mining plc. Mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada kubwa za kubadilisha mtazamo na mkakati wake mpya wa kazi yetu kubwa katika uchimbaji wa madini. Mabadiliko haya yamekuja baada ya wanahisa wa kampuni kukubaliana na kupiga kura ya kupitisha maamuzi haya jana tarehe 26 mwezi Novemba mwaka 2014.

Acacia ni mti ambao ndiyo chimbuko la jina letu jipya, ni mti unaonekana kuwa ni nembo ya mandhari ya Afrika na unaweka msisitizo kwenye malengo yetu ya kiuwekezaji Afrika. Zaidi ya hayo, tutaendelea kutumia nembo ya Afrika kwenye alama zetu zote ili kusisitiza kujikita kwetu kwenye bara la Afrika. Mfuko wetu wa Maendeleo ya Jamii wa ABG sasa utajulikana kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa Acacia.

Akizungumza kuhusu habari ya mabadiliko haya, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Acacia Mining, Brad Gordon amesema:

"Bila shaka mti wa Acacia (kwa Kishwahili "Mgunga") ni mti unaojulikana kuwa ni sehemu ya utambulisho wa mandhari ya Afrika.Kwa mikakati yetu  mipya, tutajenga biashara endelevu na yenye mafanikio makubwa nchini Tanzania na barani kote Afrika. Kama mti wenyewe wa Acacia ulivyo enea.  Tunaamini kuwa mlinganisho wetu huu na mti wa Acacia ni madhubuti na tutaweza kustahimili mazingira magumu yoyote tutakayokumbana nayo.

Tunataka kuweka wazi kuwa mabadiliko haya ya jina hayana maana kuwa ni njia ya kukwepa  wajibu waliokuwa nao ABG kama vile kulipa kodi, bali ni kuakisi hatua na mkakati wetu mpya wa biashara. Vilevile  mabadiliko haya, hayataathiri ajira zozote na hayabadilishi mfumo wa umiliki wa kampuni. Tutaendelea kuwa wachimbaji wa dhahabu tuliojitegemea na tulio orodheshwa kwenye masoko yote ya hisa ya London na Dar es Salaam.  Hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya mikataba ya ajira au makubaliano (mapatano) na masharti ya ajira katika migodi yetu kufuatia mabadiliko ya jina la Kampuni."

Kufuatia jitihada hizi za kubadilisha jina la kampuni, alama zetu kwenye  masoko ya hisa pia zimebadilika kutoka ABG na kuwa ACA katika masoko ya hisa ya London (LSE) na Dar es Salaam (DSE).

Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia iko kwenye safari kutengeneza biashara itakayo kuwa kinara  katika bara la Afrika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Ni muhimu jina hili liakisi hayo kwa usahihi.  Ubadilishaji wa jina ni hatua muhimu ya kuwaleta wadau wetu pamoja kwa lengo la kuunga mkono  utambulisho huu mpya wa kampuni.

Kampuni ya Acacia itaendelea kuwekeza na kufanya kazi kwa karibu na jamii zinazozunguka migodi yetu kupitia miradi iliyopo na miradi/mipango mipya. Tutaendelea kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa uchumi nchini Tanzania na tutaendelea kuzingatia viwango vya juu kabisa vya ubora katika biashara yetu na pia kuendeleza uchimbaji huku usalama ukiwa kipaumbele chetu muhimu.