Monday, November 10, 2014

Waziri Mkuu ataka vita dhidi ya ujangili iwe ya pamoja


Waziri Mkuu ataka vita dhidi ya ujangili iwe ya pamoja

IMG_5158

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey Mwanri mara  baada ya kuwasili kwenye makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki kufunga Mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanyamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014. Kushoto ni Waziri wa Mali asili na utalii Mh. Lazaro Nyalandu na wa pili kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu.(Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog).

* Ataka iundwe timu kufuatilia utekelezaji wa Azimio la Arusha 2014

Na Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema inahitajika dhamira ya kweli kutoka kwa wadau wote katika kutekeleza Azimio la Arusha la kukabiliana na ujangili na kuendeleza hifadhi za wanyama katika nchi za Afrika Mashariki na zilizo Kusini mwa Ikweta.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni (Jumamosi, Novemba 8, 2014) mara baada ya kufunga mkutano wa kikanda wa siku mbili uliojadili mbinu za kupambana na biashara haramu ya wanyamapori ulioandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha, Waziri Mkuu alisema: "Suala hili linataka uwajibikaji wa pamoja. Mashirika na taasisi, wananchi na viongozi sote kama wadau wakuu, kila mmoja anapaswa kushiriki vita hii kama kweli tunataka tuitokomeze."

"Kwenye hili Azimio la Arusha na nyie waaandishi wa habari pia mna sehemu yenu mmetajwa… wamesema wanatafuta jinsi ya kushirikiana na vyombo vya habari ili visaidie kutoa elimu kwa jamii kama njia ya kuelimisha umma," alisema.

Waziri Mkuu aliwaeleza waandishi hao kwamba Azimio hilo lina vipengele 20 ambavyo vinataka utekelezaji katika ngazi ya nchi mojamoja, ngazi na kanda na ngazi ya kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

IMG_5160

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akielekea kwenye chumba cha mapumziko kabla ya kufunga mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanyamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014. Kushoto ni Waziri wa Mali asili na utalii Mh. Lazaro Nyalandu, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey Mwanri na kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu.

"Nimepata faraja kwamba mkutano huu haukuisha kijumlajumla tu, bali umekuja na maazimio 20 ambayo yametengwa kwa ajili yetu sisi wa ndani, mengine yanahusisha ushirikiano wa kikanda na yako mengine yanawahusisha wadau wa maendeleo," alifafanua.

Ili kutekeleza azimio hili, nimeshauri iundwe timu itakayoshirikisha vyombo vingi zaidi badala ya kuiachia Wizara ya Maliasili na Utalii peke yake. Timu hii ikutane kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya na ikibidi Waziri atoe taarifa bungeni kuhusu utekelezaji huo," alisema Waziri Mkuu.

Mapema, akizungumza na washiriki wa mkutano huo wakati wa kuufunga, Waziri Mkuu alisema kuwepo kwa watu wa ngazi tofauti kwenye mkutano huo ni kielelezo tosha cha umakini wao na nia thabiti ya kutokomeza ujangili katika ukanda huu.

IMG_5167

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta jambo na Waziri mdogo wa Marekani anayeshughulikia Uchumi, Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli kwenye chumba maalum cha mapumziko kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufunga mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanyamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014.

"Tumeanzisha vita, tusisahau kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu na vita haijaisha. Tuzidishe mapambano katika sehemu tatu: kwenye nchi unakofanyika ujangili, nchi ambazo nyara zinapitishwa na nchi zinazopokea ama kununua hizo nyara," alisema Waziri Mkuu.

"Nakubaliana nanyi kwamba hakuna nchi inayoweza kukabili suala la ujangili ikiwa peke yake. Tunahitaji tuwe na sera mahsusi, sera ya pamoja ya kutuunganisha na kutuongoza wakati tukitekeleza Azimio hili kwa kusaidiana na wadau wa maendeleo," alisema.

Alisema Azimio hilo litaipa kazi ya ziada ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo kazi kubwa itakuwa ni kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa wa Azimio hilo unakuwa wa ufanisi.

Jumla ya nchi tisa zimetia saini azimio hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo ni Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda na Malawi.

IMG_5170

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, huku Waziri wa Mali asili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akifurahi jambo ndani ya chumba cha mapumziko kabla ya kuelekea kwenye chumba cha mikutano.

IMG_5169

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri mdogo wa Marekani anayeshughulikia Uchumi, Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli (wa pili kulia) kwenye chumba cha mapumziko baada ya kuwasili ukumbi hapo. Kushoto ni  Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez na kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu.

IMG_5182

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akibadilishana mawazo na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, kwenye chumba maalum cha mapumziko.

IMG_5253

Waziri wa Mali asili na utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akimkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda (wa pili kushoto) kufunga rasmi mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanayamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014. Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. Magese Mulongo, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Waziri mdogo wa Marekani anayeshughulikia Uchumi, Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli wakiwa meza kuu.

IMG_5264

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanayamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014 wakati akifunga rasmi mkutano huo wa siku mbili.

IMG_5198

Mwakilishi wa Balozi  wa Ufaransa nchini Tanzania akichukua taswira za baadhi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea mkutanoni hapo.

IMG_5197

Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo.

IMG_5236

Baadhi ya wawakilishi kutoka nchi tisa wakitia saini Azimio la Arusha la kukabili ujangili  mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo ni Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda na Malawi.

IMG_5205

Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa kwenye ufungaji wa mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa wanyamapori  na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014.

IMG_5224

Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke, akizungumza kwa niaba ya serikali ya Ujerumani.

IMG_5212

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta jambo na Waziri wa Mali asili na utalii, Mh. Lazaro Nyalandu wakati wa ufungaji rasmi wa mkutano huo uliodumu siku mbili jijini Arusha.

IMG_5268

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiondoka ukumbini hapo mara baada ya kuufunga rasmi mkutano huo.