Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wameaswa kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutimiza malengo ambayo Wizara imejiwekea.
Akizungumza na watumishi wa makao makuu ya Wizara hiyo jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Novemba 20, 2014), Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi amesema ushirikiano na upendo ni ngunzo muhimu za mafanikio katika taasisi yoyote.
"Watumishi wa umma, hasa tuliopo Dar es Salaam, tunatumia muda mrefu tukiwa kazini hivyo tunatakiwa tupendane na tushirikiane katika kutekeleza majukumu yetu kama timu moja," amesema Bi. Tarishi.
Katibu Mkuu huyo alikuwa alikuwa akizungumza na watumishi hao kwa mara ya kwanza tangu alipohamishiwa Wizarani hapo hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kutoka Wizara ya Mali Asili na Utalii ambako alikuwa Katibu Mkuu.
Aliongeza: "Tufanye kazi kwa malengo na kasi… tujiulize, wiki hii nimefanya nini, nimetekeleza nini," alisema kiongozi huyo na kusisitiza kuwa watumishi wa Wizara ya Katiba wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Wizara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara hiyo Bi. Theresa Mghanga alimshukuru Katibu Mkuu kwa kutenga muda kukutana na watumishi na kusisitiza umuhimu wa watumishi wote wa Wizara kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika utumishi wao.
"Tuwahi kazini na kutimiza wajibu wetu na tujione kuwa tuna deni kwa nchi yetu," alisema Bi. Theresa katika mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wote wa Wizara waliopo makao makuu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Maimuna Tarishi akiongea na wafanyakazi wa Wizara hiyo jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Nov. 20, 2014).
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Theresa Mghanga (aliyesimama) akiongea katika mkutano kati ya Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi na watumishi wa Wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Maimuna Tarishi (hayupo pichani) leo (Alhamisi, Nov. 20, 2014). (Picha na Said Benjamin).