Thursday, November 13, 2014

Rais wa Zanzibar afungua warsha ya Mahusiano ya Kisiasa na Kiutawala





Rais wa Zanzibar afungua warsha ya Mahusiano ya Kisiasa na Kiutawala
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amefungua warsha ya siku tatu kwa viongozi wa juu wa Mikoa na Wilaya kutoka Zanzibar pamoja na mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara iliyofanyika Hotel ya sea Cliff Zanzibar. Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya UONGOZI umeanza tarehe 10 Novemba, 2014. Lengo la warsha hii ni kutoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya ili kuongeza ufanisi katika utendaji. Haya yalisemwa na Profesa Joseph Semboja, Mtendaji Mkuu wa UONGOZI Institute.

Kwenye hotuba yake, Rais Ali Mohamed Shein alisisitiza umuhimu wa kuwepo mawasiliano bora baina ya viongozi na watendaji wakuu katika ngazi mbali mbali. "Mawasiliano na uhusiano ni mambo ya msingi katika utawala bora," alisema Dk. Shein, "Mategemeo yangu ni kuwa warsha hii itakupeni mbinu bora za kuimarisha uhusiano na mawasiliano kwa ajili ya kuyafanikisha majukumu yenu ya kuwatumikia wananchi."

Mh. Dk. Shein aliongezea kwamba zimekuwepo baadhi ya changamoto za mahusiano na muingiliano wa kiutendaji miongoni mwa viongozi wa kisiasa na Watendaji Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kwa hivyo ni muhimu kwa viongozi hawa kufahamu mipaka ya majukumu yao na kuwa na uhusiano mzuri kwa ajili ya utawala bora, ukuaji na maendeleo ya nchi.
Mh. Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar akitoa hotuba ya ufunguzi wa warsha ya viongozi wa juu wa mikoa na wilaya ya Zanzibar pamoja na Ruvuma, Lindi na Mtwara ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi. "Huu utakuwa ni mwanzo tu wa ushirikiano wa Taasisi ya UONGOZI, Wizara ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taasisi zetu mbali mbali," alisema Dk. Shein.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI akifungua warsha ya Mahusiano ya Kisiasa na kiutawala – Zanzibar "Warsha hii imezingatia umuhimu wa mwingiliano kati ya siasa na utendaji katika kuleta maendeleo ya nchi," Profesa Semboja alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Haji Omar Kheir, akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI.
Mh. Dk. Ali Mohamed Shein na Mh. Hawa Ghasia (MB) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wakizungumza kwenye ufunguzi.
Baadhi ya washiriki katika warsha ya "Mahusiano ya Kisiasa na kiutawala " 
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Dk. Gordon McIntosh akiendesha mafunzo haya.