Na Editha Karlo,wa blog ya jamii Kigoma
MFUKO wa Taifa wa bima ya afya umetoa jumla ya mashuka 100 kwa hospitali ya wilaya ya Kibondo mkoani kigoma ili kukabiliana na upungufu wa mashuka unaoikabili hospitali hiyo.
Akikabidhi mashuka hayo kwa uongozi wa hospitali ya wilaya ya Kibondo, meneja wa NHIF mkoa kigoma,Elius Odhiambo alisema kuwa kutolewa kwa mashuka hayo ni sehemu ya mpango wa mfuko huo katika kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya.
Odhiambo alisema kuwa mashuka hayo yaliyotolewa kwa hospitali ya wilaya ya Kibondo ni sehemu ya vifaa ambavyo vimekuwa vikitolewa kwa vituo mbalimbali vya utoaji wa huduma ya afya ambavyo vinanufaika na huduma za mfuko wa taifa wa bima ya afya.
Akipokea mashuka hayo kwa niaba ya hospitali ya wilaya ya Kibondo Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo,Emanuel Mwasulama alisema kuwa kupokewa kwa mashuka hayo kutapunguza upungufu mkubwa wa mashuka unaoikabili hospitali hiyo.
Alisema kuwa kwa sasa hali ya upatikanaji wa mashuka hospitalini hapo haiendani na mahitaji na kuomba kwamba kutolewa kwa mashuka hayo na mfuko wa Taifa wa bima ya afya iwe chache kwa wadau wengine kujitolea katika kuisadia hospitali hiyo.
Sambamba na kutolewa kwa mashuka hayo Mganga huyo wa wilaya ya kibondo alisema kuwa kumekuwa na maboresho makubwa katika utoaji wa huduma ya afya kupitia mfuko wa taifa wa bima ya afya na watu wengine wamekuwa wakieleza kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa hospitalini hapo kupitia mfuko huo.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanaopata huduma kupitia mfuko wa Taifa wa bima ya afya wamelalamikia kukosekana kwa dawa katika hospitali ya wilaya na hivyo kulazimika kufuata katika maduka ya dawa au kununua kwa pesa zao.
Akizungumzia jambo Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya kibondo, Laurean Kanaganwa amesema kuwa madawa ya shilingi milioni 44.2 yamenunuliwa na yameanza kusambazwa katika vituo vya afya na zahanati wilayani humo.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya mkoa Kigoma Elius Odhiambo (kushoto) akizungumza katika kampeni ya uhamasishaji jamii kujiunga na huduma za mfuko wa afya ya jamii (CHF) kampeni inayofanyika kwa muda wa siku 10 kwenye vijiji mbalimbali vya wilaya ya kibondo.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya mkoa Kigoma Elius Odhiambo (kulia) akikabidhi kwa Mganga Mkuu wa wilaya ya Kibondo Emanuel Mwasulama (kati kati) moja kati ya mashuka 100 ambayo mfuko huo imetoa kwa hospitali hiyo ya wilaya (kushoto0 ni Meneja wa Taifa wa mifuko ya jamii kutoka NHIF Constantine Makala (picha na Editha Karlo)