Na Mwandishi Wetu
MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bileku Mpasi, atafanya onesho maalum katika utambulisho wa nyimbo mbili mpya za bendi ya Mashujaa utakaofanyika Desemba 12 mwaka huu kwenye ukumbi wa Ten Lounge zamani Business Park.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mratibu wa onesho hilo, King Dodoo la Buche, alisema kuwa Mpasi ambaye alitamba katika tasnia ya muziki wa dansi alipokuwa na gwiji, marehemu, Pepe Kale, atakuja na wasanii wengine ili kutoa burudani ya kiwango cha juu. Dodoo alitaja nyimbo hizo mbili ambazo zitatambulishwa ni pamoja na Rafiki Sokoni na My Queen.
Aliwataka mashabiki wa muziki wa dansi nchini kujiandaa kushuhudia onyesho hilo linalotarajiwa kuwa la kihistoria hapa nchini. Rais wa Mashujaa Musica, Chalz Baba, alisema kuwa wamejiandaa kutoa burudani nzuri na kuendeleza heshima yao ya bendi bora kwa mwaka wa pili mfululizo.
" Napenda kuwahakikishia wapenzi wa bendi yetu tutafanya kazi ya ubora wa juu, ni kawaida yetu kufanya kazi nzuri, tuna usongo," alisema Chalz.
Katika onesho hilo lililodhaminiwa na Kampuni ya Mabibo Bear kupitikia kinywaji chake cha Windhoek. Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo meneja biashara wa kampuni hiyo Joseph Emmanuel, alisema wameamua kudhamini utambulisho huo ili kuendeleza muziki wa dansi nchini kufikia hadhi ya kimataifa.
Alisema kuwa wapenzi 100 wa kwanza watakaoingia kwenye onesho hilo watapewa bia moja ya Windhoek Drought bure. Mashujaa pia itatumbuiza nyimbo zake zilizotamba katika albamu zake za Risasi Kidole na Ushamba Mzigo.
Naye Rais wa Mashujaa Chalz Baba amewataka wapenzi wajiandae kupata burudani ya aina yake katika uzinduzi.
Rais wa bendi ya Mashujaa Chalz Baba, akizungumzia utambulsiho wa nyimbo zao mbili ambao utafanyika Disemba 12 mwaka huuu, kwenye Ukumbi wa Ten Lounge, utasindikizwa na mwanamuziki Bileku Mpasi kutoka nchini Congo, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Mashujaa Group, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Mabibo Bear, ambao wamedhamini onesho hilo, Picha na Mpiga Picha Wetu.