Sunday, November 23, 2014

MAREKEBISHO SHERIA YA HELSB YAONDOLEWA



MAREKEBISHO SHERIA YA HELSB YAONDOLEWA

SERIKALI imeondoa sehemu ya marekebisho ya sheria katika Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kupinga ikidai itawanyima fursa wanafunzi kutoka familia masikini kupata mikopo.



Awali, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, ulikuwa na marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo, lakini ulipowasilishwa bungeni Jumatano wiki hii, Kamati ya Huduma za Jamii, ilipinga kwa kuwa haijashirikishwa katika muswada huo.
Katika hoja yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta, alisema hawakubaliani na muswada huo kwani utawanyima fursa ya mikopo wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na uwezo.
"Sisi Kamati ya Huduma za Jamii, tunapinga muswada huu ambao utaletwa baadaye hapa baada ya kipindi cha maswali na majibu. Huu utaleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi wanaotoka familia zisizo na uwezo. "Wanafunzi elfu tisa wamekosa mikopo na wabunge wengi hapa simu zao zimejaa meseji za malalamiko ya mikopo. Hatuwezi kukaa kimya," alisema Sitta alipoomba Mwongozo wa Spika, Jumatano asubuhi.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014 bungeni juzi jioni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, haitafanyiwa marekebisho.
"Serikali baada ya majadiliano na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, imeridhia kuondoa marekebisho katika sheria hii, ili mapendekezo husika yaendelee kufanyiwa kazi zaidi kama ilivyopendekezwa na Kamati," alisema Jaji Werema.
Katika maoni yake, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria yalikusudia kuongeza makundi ya wanafunzi kuwa miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya HESLB.
Makundi yaliyokuwa yameongezwa ni wanafunzi wa Stashahada ya Juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo wanaodahiliwa katika Shuleya Sheria Tanzania.
Wengine ni wanafunzi wa Shahada ya Elimu ya Ualimu kwa masomo ya Sayansi na Hisabati na wanafunzi wa Stashahada ya Ualimu wa shule za msingi kwa masomo ya sayansi, hisabati, kusoma na kuandika