Thursday, November 27, 2014

KUMBUKUMBU


KUMBUKUMBU
MAREHEMU EMMANUEL ASUMWISYE MWASANGUTI

Mpendwa wetu EMMANUEL (Ima), Siku zimepita na hatimaye zikawa wiki, na wiki ziKawa miezi. Leo tarehe 27 Novemba 2014 unatimiza MWAKA MMOJA tangu ulipotutoka kwa majonzi makuu kwa ajali ya gari iliyotokea Dar es Salaam.

Tukikukumbuka machozi yangali yanatutiririka na kumbukumbu zingali mbichi kama vile ajali imetokea jana tu, hata hivyo tunamshukuru MUNGU mwenye uwezo wote kwa kutupigania hadi hivi leo. Kama familia tuna kumbukumbu nyingi juu yako kwa njia ya picha, utani na ucheshi wako, ndoto na matarajio yako mengi ya maisha ambavyo kwa ujumla wake tunavithamini sana. Safari yako hapa duniani japo ilikua fupi, imegusa maisha ya watu wengi na tunashukuru MUNGU kwa miaka aliyotuzawadia kuishi nawe katika familia yetu.

Kwa upendo unakumbukwa na watoto wako uliowapenda sana JOSHUA and JOEL. Joshua, ingawa taratibu anakubaliana na kutokuwepo kwako, haachi kuuliza utarudi lini! Joel, mtoto uliyemwacha akiwa angali hajazaliwa, kwa neema na rehema za MUNGU mnamo tarehe 4 Aprili, 2014 alizaliwa akiwa na afya njema, alipewa jina la Joel Asumwisye.

Unakumbukwa kwa uchungu na maumivu na wazazi wako – Asumwisye Sobha Mwasanguti na Twandege Kissale Mwasanguti, mke wako mpenzi Christabella Gonelimali, kaka na dada zako. Pia unakumbukwa na ndugu, jamaa, marafiki, majirani na pia wafanyakazi wenzako wa CRDB Bank Plc zaidi sana wale wa idara ya Treasury.

Pengo uliloliacha halitazibika kamwe. Kwa ghafla, kufumba na kufumbia ulitutoka tukibaki kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu lakini ni MUNGU pekee anayejua ni kwanini aliruhusu haya yatokee!. Ingawa hatuko pamoja nawe, roho yako itaendelea kuishi ndani ya mioyo yetu milele! Tulikupenda sana lakini MUNGU alikupenda zaidi. Katika mikono ya BWANA unapumzika, katika mioyo yetu unaishi milele! 

AMINA!