Wanazuoni, Masheikh na wazee wote nchini wana wajibu mkubwa wa kuisaidia Serikali Kuu katika jitihada zake za kukuza elimu, kujenga jamii iliyo bora, kulinda amani pamoja na kukataza maovu vikiwemo vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – hajj Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiufunguwa msikiti wa Kijiji cha Tasani Makunduchi unaokadiriwa kusaliwa na waumini wapatao 200 kwa wakati mmoja wa sala.
Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema katika msaada huo Masheikh wana fursa nzuri ya kuzungumza na waumini wao hasa kupitia hotuba za sala za ijumaa ili kujenga jamii iliyo bora.
Alisema Dini imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa zaidi kwenye suala zima la kukuza maadili mema , malezi ya watoto sambamba na kuendeleza hali ya kuishi kwa upendo miongoni mwa jamii yote.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alilifungua jengo la Madrasatul Shafiat liliopo katika Kijiji cha Kajengwa Makunduchi.
Akizungumza na waumini hao Dr. Shein alisema ufunguzi wa madrasa hiyo ni kielelezo cha jitihada za wananchi wa kajengwa kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutilia maanani haja ya kuwapatia elimu ya dini watoto wao jambo ambalo limefaradhishwa na Mwenyezi Mungu.
Alisema elimu nizawadi na urithi bora kwa watoto ambao huwajenga kuwa na ucha mungu, kujua utu, kuheshimu haki za watu wenye imani za dini nyengine sambamba na kumtukuza mola anayeteremsha neema kwa viumbe wote.
Maustadhi wa baadae wakifurahia ufunguzi wa Madrasa yao ya Shafiiyat iliyopo Tasani Makunduchi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Ustaadhati Halima Rajab Hassan akimkabidhi zawadi ya kofia ya asili ya kiua iliyoshonwa Makunduchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar mara baada ya kufungua Madrasa ya Shafiiyat ya Tasani Makunduchi.
Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar akiufungua rasmi Msikiti wa Kijiji cha Kajengwa utakaotoa huduma za ibada za sala na madrasa kwa waumini wa Kijiji hicho.
Balozi Seif akiwapongeza akina mama wa Kijiji cha Kajengwa kwa ushirikiano wao na Viongozi wao na hatimae kupelekea kupata nyumba ya ibada.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.